12 June 2012

Waziri Membe umeoneonesha ukomavu kisiasa


Na Willbroad Mathias

MWISHONI mwa wiki  Waziri wa Mambo ya Nje, Bw. Bernard Membe, aliwakaribisha nyumbani kwake viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kula nao chakula cha mchana.

Wakati wa chakula hicho alizungumza na viongozi hao masuala mbalimbali ya kisiasa ukiwemo mwenendo wa upepo wa kisiasa nchini.

Katika mazungumzo hayo Bw. Membe alikitabiria ushindi CHADEMA katika uchaguzi mkuu unaokuja na akasema kwamba chama hicho kimetokea kupendwa na wananchi katika kila kona ya nchi na hata operesheni yao ya Kusini imekitikisa chama tawala.

Viongozi hao waliookutana na Bw.Membe ni Mjumbe wa Kamati  Kuu, Bw. Godbless Lema, aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha kabla ya kuhamia CHADEMA, Bw.James Millya na viongozi wakuu waandamizi.

Waziri Membe aliwaambia viongozi hao kwamba ameishi nchi mbalimbali duniani zenye demokrasia ya hali ya juu hivyo hatashangazwa hata kidogo kama CHADEMA itaingia Ikulu.

Katika mazungumzo hayo Bw. Membe alienda mbali zaidi na kugusia  kesi iliyotengua ubunge wa Bw. Lema  ambapo alidai kushtushwa na kusema kwa vile amekata rufaa anaamini mahakama ya rufaa itamrejeshea ubunge wake.

Kwa kitendo hicho nashawishika kumpongeza  Bw.Membe  kwani  ameonesha kukomaa kisiasa na anastahili kuwa mfano wa kuigwa na wanasiasa wengine nchini.

Mbali na kumpongeza  naweza kusema kuwa ameonesha ushujaa  kwa kusema ukweli  kwani ni wachache ndani ya CCM ambao wanaweza kusimama wakaeleza ukweli huku wakifahamu chama kinakoelekea siko.

Wana CCM wenye moyo wa dhati na chama wanatambua kuwa hali ya upepo kwa sasa ndani  ya chama sio shwari kutokana na wimbi  la wanachama wake kukimbilia CHADEMA, lakini ni wachache wanaoweza kutamka hili japo  moyoni wanajua ukweli wengine wanashindwa kutamka kwa kuhofia ugali wao, wengine kuhofia posho, huku hali halisi inaonekana wazi.

Kwa kuamua kuwa muwazi, Bw.Membe ameongea yaliyo moyoni mwake na pia, ameonesha busara, hata kuna baadhi ya mawaziri na wabunge kama Ezekiel Maige amewahi kutoa kauli kama hii zaidi ya mara moja.

Na kwa kufanya hivyo, basi ni mtu mkweli asiyetaka kuficha ukweli kwa mgongo wa kukipendezesha chama kinachoshindwa kuangalia maslahi ya umma, ubinafsi na umimi, hivyo hakuna haja ya kumshambulia.

Nasema hivyo kutokana na kwamba hakuna mtu anayekuwa mtenda dhambi wa milele, isipokuwa sheteni, huongea maneno yenye upako wa Mungu, tuyaheshimu na kuyafanyia kazi kwa tahadhali ya hali ya juu.

Nashawishika kusema hivyo  kutokana na kwamba kwa hapa nchini, nina uhakika itakuwa ni mara ya kwanza kwa mbunge kuwaalika wapinzani nyumbani kwake na kuwaandalia chakula huku akiwapa maneno ya faraja kama hayo.

Hii ni kutokana na kuwa baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakichukulia siasa kama uhasama huku wakiwabeza wapinzani kwamba hawana uwezo wa kuingia Ikulu, licha ya kuelewa uwezo mkubwa waliokuwa nao baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani.

Hali hiyo imekuwa ikitokana na baadhi ya wanasiasa  kutojiamini wakidhani endapo utamkaribisha kiongozi ama mwanachama wa upinzani nyumbani kwako utakuwa unaliweka jimbo lako rehani.

Imani hiyo ndiyo imekuwa ikiwafanya baadhi ya wanasiasa  kujenga fitina miongoni mwa wafuasi wao ili wawachukie wapinzani.

Pia imani  hiyo  imekuwa ikiwafanya kujiona miungu watu huku wakiwaona wapinzani kama maadui ambao muda wote wanatishia kukitia mchanga kitumbua chao.

Kwa sasa taifa letu linakabiliwa na  hali ngumu kiuchumi iliyosababisha pia kupanda kwa gharama za maisha ,lakini wapo wapinzani ambao wamekuwa wakitoa maoni yao yenye mwelekeo wa kulinusuru taifa, lakini matokeo yake wamekuwa wakionekana kuwa maadui kwa baadhi ya wanasiasa, wakati wangeweza kuwasaidia kufikia malengo.

Nichukue fursa hii kuwaomba viongozi wengine wa siasa kulitambua jambo hilo la kuwa upinzani siyo uhasama bali ni chachu ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Viongozi wakikubali changamoto katika siasa hawataweza kuchukiana bali kujengana  kisiasa na kuongeza mshikamano baina yao.

Hii itawasaidia pia kusimama palipo na ukweli kwa maslahi ya wananchi na kuweka itikadi za kivyama mbali.

Siasa isichukuliwe kama uhasama ambao unaweza kuzaa migogoro isiyoisha, mnatakiwa kukaa pamoja na kujadili ni kwa jinsi gani mtatoa tulipo.

Hakuna kitu kinachonisikitisha ninapowaona wanasiasa wakongwe wakipanda jukwaani na kulumbana badala ya kutoa hoja za msingi kwa wananchi za utatuzi wa matatizo yaliyopo.

Tumechoshwa na siasa za uadui, siasa ni urafiki na kuiga mazuri anayofanya ama aliyofanya mwenzako hadi kukubalika na kupewa ridhaa na wananchi wake.

Hongera sana waziri Membe umekuwa  mfano wa kuigwa, wengine wafuate nyayo hizo.

8 comments:

  1. HAYATI MWL JK NYERERE NI MKATOLIKI LAKINI ALICHANGIA UJENZI WA MISIKITI YA WAISLAM HAIKUWA NA MAANA KABADILISHA DINI TATIZO LA VYOMBO VYA HABARI NI KUTOA TAFSIRI ZAO ILI KUUZA MAGAZETI WAO WAKO KIBIASHARA ZAIDI UPINZANI WANOAMINI SI UADUI WA KUTOSALIMIANA KUTOZIKANA TUNAJINGA NYUMBA MOJA YANINI KUGOMBEA FITO WANA HABARI WENGI NI WANAHARAKATI NI WAKALA WA VYAMA FULANI KILA SIKU MAKALA ZAKE NI AMA KUKOSOA TUU BILA USHAURI HAKUNA KUSIFU KUPONGEZA HAKUNA JEMA KWAO LABDA SIKU YA KIYAMA TUMEZOEA HIVYO SI AJABU WANAFADHILIWA

    ReplyDelete
  2. hii makala ni balanced na inahitaji pongezi. marekani kuna mangwiji wa siasa kwenye vyama kinzani lakini chama kinachochaguliwa hakichagui viongozi kufuatana na itikadi au misingi mingine ya kibaguzi. wanatambua lengo ni kujenga taifa na siyo kuumbuana kiitikadi na kubomoa nchi. uroho, ubinafsi, chuki, tamaa ya mali na madudu mengine yametukolea kiasi cha kuchukulia chama kama taifa!

    ReplyDelete
  3. si tujifunze tu.kutoka kwa majirani zetu hapo kenya hawana la kumuogopa mtu eti kwasababu ya kumwagiwa mboga na ugali.kile wanacho jua ni kutafuta miungano tu basi.chama hadi chama mtu hadi mtu.mimi nampongeza bwana membe kuwa, malaika wake kamwonyesha dalili za upepo wa siasa za tanzania kuwa zinabadilika.yule mtu atapenda kukilinda kiti chake cha ubunge miaka ijayo itamulazimu kujipanga kama membe kifikira kama alivyo thubutu,na lazima mwanasiasa yeyote atoke ktk uchama.na kwenda ktk muungano kama bwana membe alivyo thubutu.....mheshimiwa... iwapo kama utaendelea hivi.na hata ccm kama watakuchukia na kukutimuwa bado utakilinda kiti chako miaka miwili ijayo.kwasababu unaonyesha utanzania na sio uccm.

    ReplyDelete
  4. Mchangiaji wa kwanza umenena sawa kabisa. Shida ya magazeti ya tanzania ni kununuliwa na wanasiasa na kuandika tafsiri zao ili wauze magazeti yao, ndo mana utaona kuna uchochezi wa hali ya juu unaendelea kila kona... sasa ngoja niwaambie wahariri wa magazeti yanaondeleza uchochezi kwa mboga kidogo mnayopew... angalieni wenzenu Rwanda walivyofanywa nanyi chocheeni fujo na lazima tutawapeleka The Hague... hivi huwezi kuandika habari bila kuchochea? ua ndo shule ya journalism ya mwezi mmoja then unakuwa mhariri.....acheni upuuzi mharibu nchi bure...pumbavu..

    ReplyDelete
  5. Nadhani kuna sababu ya kutunga sheria kuwadhibit wanahabari njaa kali kama nyie wa Majira....umesikia Membe mwenyewe amekanusha yote mliyoandika.. amesema kweli aliwaita baadhi ya Chadema nyumbani kwake katika hali ya ubinadamu tu...sasa kwa vile mmepewa vijisenti na chadema muandike ili kumharibia au kuweka propaganda bila kujua mkaingia kichwakichwa....ona mlivyoaibika, Majira linaoneka kuwa ni gazeti la kidaku zaidi sasa kuliko wakati mwingine
    Kuwa makini la sivyo yatakupata yaliyompata Mwana Halisi ambalo limepoteza umaarufu kwa sababu za kijinga kama zako...kushabikia Chama...Majira na Mwananchi mko njiani kuwa Wadaku.

    ReplyDelete
  6. Bravo Kamilio Membe siku zote Mashujaa huwa hajifichi its impossible. Ulilofanya ni sahihi kabisa and no question mark.unafiki siyo mzuri sana na haujengi nakumbuka ulipoingia Bungeni ktk vipindi vyako vya kwanza ulitema cheche juu ya mke wa kigogo mmoja aliyekwenda nje kutumbua fedha za walipa kodi wa nchi hii huku akidai kwamba ni mgonjwa mwisho wa siku kigogo yule alitemeshwa mzigo kwa sababu mzee Mkapa alipenda tu aelezwe ukweli usiokuwa na doubt,Leo hii umeonyesha tena sura yako kwamba wewe siyo mnafiki na watu wakijua kufanya kazi wape haki yao Usikalie mambo ya Wassira Stephen na Lukuvi wanachosha watanzania walio wengi, Bravo Man.

    ReplyDelete
  7. Kuna viongozi wachache waliotukuka katika CCM na nadhani Mh. Membe ni mmojawapo....wanasiasa wanatkiwa kujua kuwa siasa za vyama vingi sio vita bali ni msingi wa kuleta uwiano katika mwenendo wa taifa katika kushughulikia masuala ya nchi kwa hekima ambazo zitafanya wananchi kuneemeka

    ReplyDelete