01 June 2012
Washauriwa kuwajengea uwezo watoto yatima
Richard Konga na Queen Lema, Arusha
JAMII zimeshauriwa kuachana na uchangiaji wa shughuli za hanasa badala yake ijikite zaidi kuyajali makundi yasiyojiweza hususan watoto yatima na wenye maambukizi ya Ukimwi wanaolelewa bila msaada wa uhakika kwenye vituo vya watoto yatima.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Kikundi cha Mshikamano cha jijini Arusha Bw. Godilizeni Temba wakati kikundi hicho kilipotembelea na kutoa msaada wa vyakula na vinywaji wenye thamani ya shilingi milioni moja kwa vituo viwili vya kulelea watoto yatima mjini hapa.
Vituo hivyo ni pamoja na Sant Lusia kilichopo Moshono kinacholea watoto wenye maambukizi ya ukimwi pekee na Kituo cha Sant Joseph kilichopo Kata ya Mlangarini wilayani Arumeru.
Bw. Temba aliwaomba Watanzania kujijengea utaratibu wa kujisaidia wenyewe na kuachana na dhana iliyojijenga ya kutegemea wafadhili pekee kutoka nje ya nchi ambao wengi wao wamekuwa wababaishaji huku wakiweka masharti magumu na misaada yao.
Aidha, alisema jamii ina kila sababu ya kuguswa na tabu wanayoipata watoto yatima kwani mbali na kukabiliwa na changamoto nyingi kimaisha wamekosa msaada muhimu ya kijikimu hususan elimu bora itakayowasaidia kuondokana na utegemezi hapo baadaye.
Pia alitoa rai kwa kila Mtanzania kwamba jukumu la kuyasaidia makundi hayo ni wajibu wa kila mtu iwapo ataguswa na kujitolewa hata kwa kuchangia mtoto mmoja kila mwaka ikiwepo kumsombesha na kuachana na uchangiaji mkubwa wa hanasa ambao umekuwa ukipoteza fedha nyingi kwa muda mfupi.
"Suala la kuwasaidia watoto ni jukumu la kila mtu ni vizuri basi kwa kila Mtanzania, iwapo ataguswa kwa namna yake na kutoa mchango kwani wengi wetu tumekuwa tukijitoa sana kuchangia harusi za kifahari, bila kujali kuwa michango yetu pia inahitajika kwa makundi mengine muhimu," alisema
Naye Mkuu wa Kituo cha Watoto Yatima cha St.Lucia Bi. Winfrida Mrema alisema kuwa kituo chake kinalea watoto wenye umri wa miaka mwili hadi 10 wenye maambukizi ya VVU na kimekuwa kikikabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa lishe bora kwa watoto hao.
Aidha, kwa upande wa mmiliki wa Kituo cha St.Joseph Sister Crispin Mnate alisema kuwa kituo hicho kina jumla ya watoto yatima 46 na wamekuwa wakilelewa katika mazingira magumu kutokana na kukosa ufadhili wa kudumu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment