12 June 2012
Stars, Gambia zaingiza mil. 124/-
Na Zahoro Mlanzi
MCHEZO wa timu ya Taifa (Kilimanjaro Taifa Stars) na Gambia, uliochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, umeingiza sh. 124,038,000.
Mechi hiyo ilikuwa ni ya Kundi D ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil, ambapo wenyeji Kilimanjaro Taifa Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Timu zingine za kundi hilo ni Ivory Coast na Morocco, ambazo nazo zilifungana kwa mabao 2-2.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura ilieleza kwamba mapato hayo yametokana na washabiki 31,122 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo.
"Asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni sh. 18,921,050.85 ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa (sh. 6,555,000) na bonasi kwa Taifa Stars (sh. 15,767,542.37)," alisema Wambura.
Alisema waamuzi sh. 13,372,000, usafi na ulinzi sh. 2,350,000, maandalizi ya uwanja ni sh. 400,000, Wachina ni sh. 2,000,000, umeme sh. 300,000 na mafuta ya jenereta sh. 200,000.
Aliongeza kwa upande wa mgawo asilimia 20 ya gharama za mechi ni sh. 12,834,481, asilimia 10 ya uwanja sh. 6,417,241, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 3,208,620, asilimia 20 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 12,834,481 na asilimia 45 ya TFF (sh. 28,877,583).
Wakati huohuo, Waamuzi 54 wameanza kozi ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Wambura, alisema kozi hiyo itamalizika Juni 14, mwaka huu na inaendeshwa na wakufunzi wawili kutoka FIFA wakisaidiwa na wakufunzi wengine wanne wa TFF. Wakufunzi wa FIFA ni Carlos Henriques na Mark Mizengo.
Wakufunzi kutoka TFF ni Kapteni mstaafu Stanley Lugenge, Leslie Liunda, Soud Abdi na Riziki Majala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment