11 June 2012

SBL yadhamini ngoma za Bulabo



Na Daud Magesa, Mwanza

NGOMA za utamaduni za asili ya kabila la Wasukuma ‘Bulabo’, zimepata udhamini wa sh. milioni 12 kutoka Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kupitia bia ya Serengeti.

Ngoma hizo za asili hushindanisha vikundi vya Wagika na Wagaru vya kabila hilo, katika kuadhimisha na kusherehekea mavuno kila mwaka, zitashirikisha vikundi 30 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkurugenzi wa Idara ya Masoko ya SBL, Ephraem Mafuru alisema udhamini huo ni kwa ajili ya kuwezesha washiriki wa tamasha hilo la ngoma za asili za Bulabo mwaka huu.

Alisema udhamini huo ni kwa ajili ya gharama za usafiri, vifaa vitakavyotumika, malazi pamoja na chakula kwa vikundi vyote 30 ambavyo vitashiriki tamasha hilo.

Mafuru alisma udhamini huo ni kutambua mchango wa kabila la Wasukuma katika kuendelea utamaduni wao, pamoja na kutangaza utalii wa ndani unaoelekea kupotea kwa kupitia ngoma za Bulabo, ili kuhamasisha makabila mengine kufanya shughuli za utamaduni wao.

“Musimu wa sherehe za mavuno kwetu ni mwonekano wa dhahabu na bia yetu ya Serengeti imekuwa pamoja nao katika kusherehekea mavuno na kuendeleza mila na desturi za kabila la Wasukuma, ambazo huambatana na sherehe za mavuno kwa kabila hilo,” alisema.

Alisema SBL itaendelea kuangalia sekta ya utamaduni wa makabila mbalimbali ya Tanzania, ili kuyahamasisha kuenzi tamaduni zao kwa kutangaza utalii wa ndani lakini pia ukilenga kuendeleza kizazi hadi kizazi, kwa vile utalii wa ndani una uwezo wa kuendeleza utamaduni wetu.

Ngoma za Bulabo zilianza mwaka 1700 kabla ya kuboreshwa na kuingizwa katika Kanisa Katoliki mwaka 1954, ambapo ngoma hizo za asili zilichezwa na kushindanisha makabila ya Wagika na Wagalu.

No comments:

Post a Comment