08 June 2012

Ratiba ya Copa Coca-Cola yatolewa



Na Elizabeth Mayemba

DROO ya mashindano ya vijana chini ya miaka 17 ya Copa Coca-Cola Ngazi ya Taifa ilichezeshwa jana na tayari ratiba ya mashindano hayo imetolewa.

Mashindano hayo yanatarajia kuanza kutimua vumbi Juni 24, mwaka huu katika viwanja vinne jijini Dar es Salaam, huku kila kundi likiwa na timu saba.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa mashindano hayo ya vijana Msafiri Mgoi, alisema wameamua kuchezesha droo hiyo ili isionekane kama wamepanga ratiba kwa kuzipendelea timu fulani.

"Kila mtu ameshuhudia droo jinsi ilivyochezeshwa, hivyo hakuna upendeleo wowote ni wajibu wa makocha kuleta wachezaji ambao watakidhi vigezo hasa suala la umri, na timu itakayokiuka vigezo kuna adhabu ambayo itatolewa," alisema Mgoi.

Alisema timu zote zinatakiwa kuwasilisha usajili kwa muda unaotakiwa na pia ana imani udanganyifu hautakuwepo katika suala zima la umri, ili mashindano hayo yafanyike kwa haki.

Mgoi alisema Kundi A lina timu za Kigoma, Lindi, Ilala, Arusha, Kusini Pemba, Rukwa na Ruvuma katika ambapo timu zitafungua dimba ni Kigoma na Lindi ambazo watacheza Uwanja wa Karume.

Alisema Kundi B lina timu za Morogoro, Manyara, Kaskazini Magharibi, Mjini Magharibi, Iringa, Mwanza na Tanga na timu zitakazofungua dimba ni Morogoro na Manyara kwenye Uwanja wa Kawe.

Mwenyekiti huyo alisema Kundi C lina timu za Temeke, Kinondoni, Mtwara, Mbeya, Kaskazini Unguja, Dodoma na Mara na watakaofungua dimba ni Temeke na Kinondoni kwenye Uwanja wa Nyumbu.

Alisema Kundi D lina timu za Kilimanjaro, Kusini Unguja, Pwani, Singida, Shinyanga, Kagera na Tabora, watakaofungua dimba ni Kilimanjaro na Kusini Unguja kwenye Uwanja wa Tamko.

No comments:

Post a Comment