13 June 2012

Miss Kigamboni kufanyiwa usaili leo



Na Zahoro Mlanzi

WAREMBO 12 wanaotarajia kuwania taji la kitongoji cha Kigamboni, mwaka huu 'Miss Kigamboni City 2012', leo wanatarajiwa kufanyiwa usaili kwa ajili kumpata mshindi wa shindano hilo litakalofanyika Ijumaa kwenye Ukumbi wa Navy Beach, Dar es Salaam.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa shindano hilo, kutoka Kampuni ya K&L Media Solutions, Somoe Ng'itu, alisema maandalizi ya zoezi hilo yamekamilika na wanachosubiri ni siku ya shindano ifike.

Alisema kitongoji hicho kina warembo wenye sifa na wanaojiamini ambao wamepania kurudisha taji la Miss Tanzania kwenye Kanda ya Temeke.

Aliongeza ili kuboresha shindano hilo Bendi ya Muziki wa Dansi ya FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma' na msanii na mchekeshaji mahiri hapa nchini, Mpoki watatumbuiza kwenye kinyang'anyiro hicho.

"Tunawaomba wadau wa sanaa ya urembo kufika kushuhudia mrembo wa Kigamboni atakavyopatikana, ni Kitongoji kilichoko sehemu pekee hapa nchini, hivyo ni vizuru kushuhudia shindano hilo," alisema Somoe.

Aliwataja warembo watakaochuana ni Susanne Jeremiah, Agness Goodluck, Elizabeth Boniface, Dorothea Kessy, Esther Albert, Edda Silyvester, Sophia Martin, Doreen Kweka, Khadija Kombo, Linnah David, Rosemary Peter na Winnie Karaya.

Aliwashukuru wadhamini ambao wamejitokeza kusaidia shindano hilo ambao ni Redd's, Dodoma Wine, hoteli ya Hope Country, Screen Masters, Global Publishers, Nobro Collections, Times FM na Clouds FM.

Aliongeza kuwa warembo watakaoshika nafasi tatu za juu kutoka katika shindano hilo wataungana na wenzao kutoka vitongoji vya Kurasini na Chang'ombe ili kuwania taji la Kanda ya Temeke baadaye mwaka huu.

No comments:

Post a Comment