14 June 2012

KCBL yaanzisha akiba mpya kwa watoto chini ya miaka 18


Na Heckton Chuwa, Same

BENKI ya Ushirika mkoani Kilimanjaro (KCBL), imeanzisha huduma ya akiba kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ili waweze kupata uelewa wa huduma za kibenki.

Meneja Masoko wa benki hiyo Bw. Ahsanterabi Msigomba, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa Vyama vya Ushirika vya Msingi na wale wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya za Mwanga na Same (VUASU).


“Huduma hii inalenga kuwajengea watoto mazingira ya kuanza kuwa na uelewa wa kujiwekea akiba tangu utotoni,” alisema Bw. Msigomba na kuongeza kuwa, benki hiyo pia imeshirikiana na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kwa kuanzisha huduma ya M-PESA na wao kuwa wakala wa huduma hiyo.

“Huduma hizi nyongeza ya huduma zingine tunazozitoa ambazo ni pamoja na zile za Western Money Union Transfer na stakabadhi ya mazao ghalani ambazo zimekuwa na mafaniko makubwa,” alisema.

Bw. Msigomba alisema mpango wa stakabadhi ya mazao ghalani umeendelea kuwa na mafanikio makubwa tangu uanzishwe kutokana na huduma wanazotoa kwa wakulima ambao hawana rasilimali zinazowapa uwezo wa kukopa fedha kwa ajili ya kilimo.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa benki hiyo Bi. Regina Ndesanjo, alitoa wito kwa wanachama wa benki hiyo kukamilisha hisa zao ili zifikie kiwango cha milioni moja ambacho kimewekwa ili waweze kushiriki Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.

No comments:

Post a Comment