28 May 2012

Zanzibar yatwaa ubingwa wa judo Taifa


Na Amina Athumani

ZANZIBAR imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Judo katika michuano ya Taifa ya mchezo huo iliyomalizika jana katika Ukumbi wa Land Mark Hotel, Dar es Salaam.

Zanzibar ambao pia ni mabingwa wa Afrika Mashariki katika mchezo huo wamefanikiwa kutwaa ushindi wa jumla katika michuano hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Judo Tanzania Bara (JATA).

Michuano hiyo ambayo imeanza juzi ilishirikisha wachezaji kutoka Zanzibar na Tanzania Bara ambayo ilikuwa ikiwakilishwa na timu kutoka mikoa na klabu mbalimbali.

Kwa upande wa washindi mmoja mmoja, Ahmed Magongo kutoka Korogwe, Tanga amenyakua ubingwa wa jumla na kufanikiwa kupata kitita cha dola za marekani 1,000 zilizotolewa na mdhamini Gemin.

Pia kwa upande wa washindi wa uzito wa juu mchezaji Masoud Amour kutoka Zanzibar  anayecheza uzito wa kilo 100 amefanikiwa kukaa kileleni katika uzito huo.

Mohamed Hamis kutoka Zanzibar aliyepigana katika uzito wa kilo 81, amefanikiwa kukaa kileleni ambapo kwa upande wa wanawake mchezaji Matilda Mgasi anayecheza kilo 63 ameshika nafasi ya kwanza katika uzito wake.

Akizungumzia mashindano hayo, Mwenyekiti WA JATA, Chief Kiumbe alisema mashindano hayo ni mara ya kwanza kufanyika kwa wachezaji kupewa fedha taslim.

Alisema kupitia mdhamini wao Genim wamefanikiwa kuyafanya mashindano kuwa katika ubora wa hali ya juu na kuomba wadau, Kampuni na taasisi binfsi kuunga mkono maendeleo ya mchezo huo kwa kutoa sapoti katika mashindano mbalimbali watakayoyaandaa.

Alisema changamoto kubwa inayoikabili JATA hadi sasa ni kukosekana kwa ukumbi wa kudumu wa kuchezewa mchezo huo na kwamba Zanzibar wamekuwa wakifanya vema katika mashindano mbalimbali ya Afrika kutokana na kuwa na ukumbi mkubwa kwa ajili ya mchezo huo.

No comments:

Post a Comment