15 May 2012
Wafanyabiashara soko la Tandale waililia Masasi
Na Hamisi Nasiri, Masasi
WAFANYABIASHARA wa mboga mboga katika Soko la Tandale Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wameiomba Hamalshauri ya wilaya ya Masasi kuboresha eneo wanalofanyia biashara kutokana na adha wanayopata wakati wa mvua za masika
.
Katika mahojiano na gazeti hili kwa nyakati tofauti wafanyabiashara hao walisema wamekuwa wakifanya biashara katika mazingira magumu kutokana na mabanda yao wanayofanyia biashara kuezekwa kwa maboksi¸ magunia pamoja na nailoni ambazo wakati wa mvua huvuja.
Bi. Maliamu Selemani mfanyabiashara sokoni hapo kwa zaidi ya miaka 10 alisema, halmashauri wakiboresha soko hilo anaamini wafanyabiashara wengi zaidi wangehamia kufanya biashara hapo na hivyo soko hilo kupanuka zaidi na pia ingesaidia kuongeza idadi ya wateja wa soko hilo.
Alisema, ni bora halmashauri wakaboresha eneo hilo kwa kuwajengea mabanda yaliyo na ubora na si kama ilivyo hivi sasa ambapo inawalazimu kutandika maboksi pamoja na magunia na kisha kupanga bidhaa na wengine wamekuwa wakiuzia bidhaa zao chini hali ambapo inahatarisha afya za walaji wanaokwenda kununua bidhaa katika soko hilo.
Alisema kuwa, ¸wengi wao wapo katika soko hilo zaidi ya miaka 15 lakini hakuna maboresho yoyote ambayo yanafanyika katika kuhakikisha wafanyabiashara wa soko hilo wanakuwa na sehemu mzuri ya kufanyia shughuli zao licha ya kutoa malalamiko ya mara kwa mara kwa halmashauri kuboresha eneo hilo la biashara.
“Tunaiomba hamalshauri yetu kulipa kipaumbele suala la kuboresha eneo hili kwa kuwa wafanyabiashara wa hapa tunafanya biashara katika mazingira magumu sana kiabiashara wakati hili soko ni kubwa hapa wilayani…lakini hapa sokoni kwetu hakuna hata tundu moja la choo jambo ambalo kiafya ni hatari¸” alisema Bi.Selemani
Kwa upande wake Bw.Hamisi Kambona alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri kuboreshwa kwa maeneo wanayofanyia biashara bila mafanikio hali inayowafanya wafanye shughuli zao katika mazingira hatarishi hasa kipindi cha mvua za masika ambapo harufu huwa mbaya inayotokana na mazalia ya uchafu yaliyo katika soko hilo.
Alisema, halmashauri imekuwa ikiwatoza ushuru wa soko wafanyabiashara hao wa sh. 200 kwa siku kwa kila mfanyabiashara huku wakijuwa mazingira ya soko hilo yakiendelea kuwa mabaya ambapo ukilinganisha na kiwango wanachotozwa hakiendani na mazingira ya soko yalivyopo.
“Kwa kweli miundombinu ya hapa kama unavyoiyona mabanda mengi yameezekwa kwa magunia pamoja na nailoni na hata wengine wanapanga bidhaa zao chini, cha msingi ni kwamba hapa halmashauri lazima iwe na mkakati mahususi wa kuboresha hili soko ili wafanya biashara tufanyebiashara mazingira yaliyo bora¸” alisema
Kwa upande wake Mwenyikiti wa soko hilo Bw. Mohamedi Mtahungo alisema suala la kuboreshwa kwa soko hilo ni kitu cha msingi kwani mazingira yaliyopo hivi sasa ni magumu ikilinganishwa na shughuli zinazofanywa na wafanyabiashara wa soko hilo.
“Tumeshawaeleza mara kadhaa halmashauri ya wilaya kutuboreshea miundombinu ya soko letu, lakini hatujapewa majibu ya kuridhisha na tulipohoji tuliezwa kuwa soko hili halipo katika eneo husika kwa shughuli za biashara na hata eneo ambalo walituonesha kuwa ni eneo maalumu la kufanyia biashara zetu tulipokwenda huko tumekuta ujenzi wa makazi ya watu ukiendelea kufanyika hivyo hatujuwi nini chakufanya¸” alisema Bw. Mtahugo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment