10 May 2012

Wafanyabiashara msiruhusu vitendo vya rushwa '


Na Jovin Mihambi,
Mwanza

WAFANYABIASHARA katika sekta binafsi wameshauriwa kutoruhusu vitendo vya rushwa
vinavyotokana na ushawishi kutoka kwa baadhi ya watumishi wa serikali ambao wamepewa
dhamana kusimamia manunuzi au tenda za serikali.


Hayo yalielezwa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikillo
katika hotuba yake aliyoitoa kwa washiriki wa mafunzo ya siku mbili juu ya utawala
bora katika biashara kwa washiriki kutoka sekta binafsi iliyofanyika  jijini Mwanza.

Alisema kuwa sekta binafsi nayo imepewa nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo ya
taifa kutokakana kwamba fedha zinazotengwa na serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, zinapitia katika halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji kwenda kwa wafanyabiashara katika sekta binafsi ambao hupewa tenda kwa ajili ya miradi ya maendeleo nchini.

Alisema kuwa kutokana na baadhi ya watumishi serikalini ambao wamepewa dhamana ya
kusimamia fedha hizo na kuzigawa kwa wafanyabiashara kwa ajili ya kuendeleza miradi
ya maendeleo, baadhi ya fedha hizo huchukuliwa na baadhi ya watumishi wa serikali
wasio waaminifu kupitia kwa wafanyabiashara hao ikiwa ni rushwa kwa ajili ya kupewa
asante ya kupewa fedha hizo kwa ajili ya miradi husika.

"Matokeo yake, miradi hiyo inakuwa haikidhi viwango kutokana kwamba fedha hizo
zinazotolewa kwa watumishi hao kama rushwa, mwenye tenda hufanya kazi chini ya
kiwango ili kufidia pengo hilo na wakati mwingine mwenye tenda hukimbia kazi
aliyopewa kutokana na yeye kujichukulia jukumu la kutumia kiasi chote cha fedha kwa
 manufaa yake," alisema

Alisema kuwa serikali kwa kutambua kuwa sekta binafsi nayo imo katika mchakato wa
kuzuia na kupambana na rushwa, imeamua kuijengea uwezo sekta hiyo ili kuweza
kutambua wajibu na majukumu ya kupambana na vitendo vya rushwa pamoja na kupata
mbinu shirikishi za kukabiliana na rushwa kwa kupitia mafunzo ya utawala bora katika
biashara.

"Msiwaonee haya wale ambao hawafuati maadili kwenye sekta yenu, waelewesheni wajibu
wao na kuwachukulia hatua za kinidhamu wale ambao hawatapenda kuwaelewa na kama
mtapata ushahidi wa kutosha kwamba toeni taarifa TAKUKURU" alisema Injinia Ndikillo.

Mafunzo hayo yalishirikisha wafanyabiashara 40 kutoka sekta binafsi kutoka wilaya za
Mkoa wa Mwanza ikiwa ni mkakati wa kutoa mafunzo kwa sekta hiyo kwa ajili ya
mapambano dhidi ya rushwa nchini awamu ya pili (NACSAP 11) na kuratibiwa na Ofisi ya
TAKUKURU Mkoa wa Mwanza.

No comments:

Post a Comment