28 May 2012

Uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia 6.4 mwaka 2011'





Na Pendo Mtibuche, Dodoma

UCHUMI wa Tanzania umekua kwa asilimia 6.4 mwaka 2011 ambapo katika sekta ya usafirishaji na mawasiliano, ukuaji huo upo asilimia 11.3.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Beno Ndulu aliyasema hayo mjini Dodoma mwishoni mwa wiki wakati akitoa mada katika mafunzo elekezi yanayoshirikisha wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wa mikoa.


Alisema, uchumi katika sekta ya fedha umekua kwa asilimia 10.7, ujenzi 9.0, biashara 8.1 na uzalishaji 7.8 ambapo hadi sasa, Tanzania inakopesheka kinyume na taarifa zinazotolewa ambazo si rasmi.

Alisema, sekta ya kilimo bado inaongoza katika kuliingizia Taifa ikifuatiwa na biashara, uzalishaji na ujenzi.

Pia Gavana huyo aliishauri Hifadhi ya Taifa ya Chakula kuanza kuwa na mkakati wa kuhifadhi mpunga badala ya mahindi pekee ili kupunguza mfumuko wa bei kwani mchele ni nafaka inayotumiwa sana na kaya mbalimbali.

Hata hivyo Prof. Ndulu alisema kushuka kwa thamani ya fedha nchini kumepungua kutoka asilimia 19.7 hadi 19.0 mwaka 2002.

“Kushuka kwa thamani ya fedha, kumetokana na kushuka kwa bei ya bidhaa hasa katika eneo la nishati na mafuta hadi sasa asilimia 75 ya Watanzania wanategemea kilimo hivyo ili Tanzania iweze kupiga hatua katika maendeleo, sekta hii inatakiwa kutiliwa mkazo,” alisema Prof. Ndulu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Tume ya Mipango Dkt. Phillip Mpango aliwataka viongozi kuongoza kwa mifano badala ya nadharia ili kujua changamoto zinazowapata wale wanaowaongoza.

Aliwataka viongozi kuwa na uchungu na uduni wa maisha ya wananchi wengi wanaowaongoza, kuangalia namna ya kuwasaidia ili waweze kuondokana na matatizo yanayowakabili.

Mafunzo hayo yanahudhuriwa na Wakuu wa Mikoa 24, Makatibu Tawala wa Mikoa 25 na Wakuu wa Wilaya 133

No comments:

Post a Comment