14 May 2012

NCCR-Mageuzi wapata pigo, Athanasi ajivua kundini


Na Anneth Kagenda

ALIYEKUWA mgombea Ubunge Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi Bw. Mawazo Athanasi amejiondoa kwenye chama hicho kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kukosa imani na Mwenyekiti wake Bw. James Mbatia.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam mara baada ya kufika jijini hapa akitokea Kigoma, alisema kuwa amechukua maamuzi hayo magumu kutokana na mwenyekiti wake kuwa mwanachama wa CCM kutokana na kwamba kama angekuwa ni mwanachama wa NCCR- Mageuzi asingekubali kupewa cheo cha wanawake wa CCM (Viti Maalum).

"Awali tulikuwa tunajiuliza maswali mengi kwamba Bw. Mbatia ni wa chama chetu au CCM...sasa ukweli tumeupata kwamba ni wa CCM, pia ninajiuliza kama angekuwa na nia ya dhati na chama basi angekataa cheo hicho ambacho ni cha wanawake wa viti maalum CCM, lakini ninajiuliza je? Huko bungeni anaenda kufanya nini na anakitetea chama gani.

"Niko katika chama hiki tangu mwaka 2003, lakini nilikuwa nashangazwa na mwenendo wa chama changu, baada ya kuona mambo yanazidi kuharibika ngoja nikae pembeni kwani chama hiki hiki kilishindwa kunitetea hata nilipokuwa nashughulikia kesi yangu ambapo nilishindwa kutimiza masharti ya kupeleka sh. milioni tano mahakamani wakati milioni mbili zilikuwa zimepatikana, lakini nikakosa milioni tatu," alisema.

Aidha, alisema kuwa awali Bw. Mbatia alimwambia (Bw. Athanasi) kwamba aachane na kesi hiyo ambayo aliamini kwamba angeshinda kutokana na kwamba aliibuka kidedea cha mshindi wa pili na kwamba kura zake ziliibiwa na Bw. Christopher Chiza wa CCM ambapo alisema kuwa kitendo hicho cha kuhujumiwa na chama chake hakukifurahia.

Alisema, pia anakubali uteuzi wa Rais wakati akijua kuwa tayari alimteua mwizi wa kura zake (Chiza) kuwa Waziri na kusema kuwa iweje ampende Bw. Mbatia wakati anajua kuwa aliwaibia kura katika Jimbo la Buyungu na kusema kuwa kilichoendelea kumuudhi ni viongozi wa NCCR-Mageuzi kuunga mkono uteuzi wa Bw. Mbatia.

Hata hivyo aliwataka vijana wote wa mkoani Kigoma ambao wako kwenye chama alichokihama kuondoka mara moja kwa madai kuwa chama hicho kinakufa na kuwa CCM kwani viongozi wake wataendelea kuongopewa kwa kupewa vyeo na Rais Jakaya Kikwete.

No comments:

Post a Comment