08 May 2012

Mawaziri waliojiuzulu wazidi kukabwa koo



Na Gladness Mboma


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini Bw. Zitto Kabwe, amesema watamshangaa Rais Jakaya kikwete, kama hatamchukulia hatua za haraka kwa kumfikisha mahakamani aliyekuwa Waziri wa Fedha, Bw. Mustapha Mkulo na wenzake, waliotuhumiwa moja kwa moja na wabunge kwa ubadhirifu.


Bw.Zitto alitoa kauli hiyo jana kwenye viwanja vya Ikulu, ambapo alishiriki tukio la kuapishwa kwa mawaziri na manaibu waziri.

"Kuna wale waliotuhumiwa moja kwa moja kama vile Mkulo, tunataka ndani ya muda mfupi Rais atawafikisha mahakamani,"alisema Bw. Zitto ambaye juzi aliwatahadharisha Mawaziri kutofanya sherehe na kuvishwa maua wakati watakapoapishwa, alisema kuwa wapo mawaziri waliokwenda na maua hayo, lakini yalikataliwa getini.

Katika tukio la jana hakuna waziri aliyevalishwa taji la maua baada ya kuapishwa na ndugu wa karibu, lakini hakuna ushahidi kuwa yalizuiliwa mlango wa kuingilia Ikulu kama alivyodai Bw. Zitto.

Alisema kwamba sasa wana kazi ya kusimamia Serikali ili iendelee kuwawajibisha wale wote wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa mali ya umma.

Bw. Zitto alisema kuna watu ambao hawana makosa, ila kosa lao limesababishwa na watendaji wa chini, hivyo inabidi Rais Jakaya Kikwete ashikilie msimamo wake wa kuwawajibisha wale watendaji wote waliosababisha hasara kwa umma. 

Alisema kuwa wamedhihirisha kwamba bunge lina uwezo wa kung'ata na halina meno ya plastiki na kwamba uteuzi wa mawaziri hao umetokana na shinikizo lao.

No comments:

Post a Comment