17 May 2012

Manispaa ya Bukoba na mikakati ya kuendeleza wananchi kiuchumi



Na Anneth Kagenda

TATIZO la ajira kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa limeendelea kuwa sugu nchini huku idadi ya watanzania ikifikia milioni 42 hali inayoweza kuwa mbaya zaidi baada ya mika mitano.

Pia, umaskini umeshika kasi Tanzania licha ya kuwa na rasilimali nyingi, ikiwamo ardhi yenye rutuba, bahari, mito na maziwa, madini na wanyamapori.

Ongezeko la watu nchini haliendani na maendeleo ya kiuchumi na kusababisha umaskini hasa kwa vijana kuwa kubwa kuliko jitihada za kulimaliza tatizo hilo.

Kila mwaka vijana 8000 wanaomaliza katika vyuo vya ualimu nchini hupokelewa ajili ya kupewa ajira za ualimu pamoja na kwamba bado hazitoshi.

Utoaji wa ajira hizo ni lengo la serikali ambayo imekuwa ikitaka kumaliza tatizo hilo kwa vijana pamoja na kwamba jitihada hizo bado hazijakidhi mahitaji kwa walengwa.

Kutokana na kuwapo kwa tatizo la ajira nchini na kwa baadhi ya nchi nyingine duniani,  ajira zinazotolewa na serikali huwa hazikidhi mahitaji ya walengwa.

Pia tatizo la ukosefu wa ajira limekuwa likiongezeka kila mwaka hususan mjini kutokana na vijana wengi kukimbia vijijini kufuata huduma muhimu za jamii.

Wengi wao hukimbilia mijini kwa kudhani kwamba wanaweza kupata ajira kirahisi jambo ambalo sio kweli na badala yake huishia katika makundi ya uhalifu na vijiweni wakipiga debe.

Katika kukabiliana na changamoto hii, serikali haiko peke yake badala yake ina wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambao hawapendi kuona vijana wakizurura na kushinda vijiweni.

Taasisi na wadau hao wamekuwa wakijitahidi kutafuta miradi, kwenye viwanda na maeneo mengine ili vijana wajishughulishe wakati wote pamoja na kwamba jitihada hizo bado zinaendelea kutokana na kwamba mahitaji bado ni makubwa.

Meya wa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera Dkt. Antony Amani, anasema, baada ya kuona tatizo hilo limekithiri aliamua kutafuta mbinu kupambana nalo.

Anasema, baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo mwaka 2011 alikumbana na changamoto nyingi na kubwa ambazo alitakiwa kuhakikisha zinapungua kama siyo kuisha kabisa.

"Changamoto ya kwanza niliyokumbana nayo uso kwa uso na ikanishangaza ni ile ya upungufu wa watu wenye hati za kumiliki ardhi ambapo tangu dunia inaumbwa nilikuta idadi ikiwa ni watu 4,881 wenye hati za kumiliki ardhi," anasema Dkt. Amani.

Anasema kuwa, kwa uzoefu wa siku nyingi alionao hakutegemea Manispaa kama hiyo kubwa iwe na hati kidogo kiasi hicho hivyo kujiapiza kwamba suala hilo lazima alivalie njuga.

"Na cha kushangaza zaidi kumbe kuna watu waliowahi kulizwa na wajanja wa mjini ambapo mwaka 2003 waliambiwa kwamba watu 8000 watapewa viwanja kumbe ulikuwa uongo," anasema.

Anaeleza kuwa, mgogoro huo uliodumu kwa miaka 8 huku mapato ya ndani yakiwa ni milioni 9 kwa mwaka.

Anasema kuwa, aliamua kuungana na  watendaji kuingia kwenye mkakati wa kuanza kutafuta fedha kwa lengo la kuanza rasmi kupima viwanja na ambapo jumla ya sh. bilioni 2.9 zilipatikana kutoka Unity Trast Of Tanzania (UTT).

"Fedha hizi zilipatikana na tukaanza kulipa fidia na kupata viwanja, kutengeneza barabara katika maeneo ambayo viwanja vinapimwa ili paweze kufikika kwa haraka," anasema Meya huyo.

Anasema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kupima viwanja 5000 ndani ya miaka miwili na kuwakabidhi wananchi hati zao ili wapate mikopo kupitia hati hizo.

Anasema, zoezi hilo linaendelea vizuri na watu wanaendelea kununua viwanja huku barabara zikiendelea kutengenezwa katika maeneo yote ya Manispaa yake kuzunguka mji wa Bukoba.

Anasema kuwa, changamoto nyingini ni ile ya mapato kidogo ambapo alisema kuwa baada ya kuliona hilo alitambua wazi kwamba tatizo linatokana na wawekezaji kuwa wachache hivyo ameanza maongezi  na mashirika mbalimbali pamoja na taasisi.

"Nilizungumza na shirika la Nyumba NHC, PPT na PSPF na kuyashawishi yajenge nyumba ili kuwakopeshe wananchi wote ambao watalipa kwa awamu kadhaa na ndani ya miaka miwili  mambo yatakuwa mazuri," anasema  Dkt. Amani.

Anasema, katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa ajira, amelenga kukuza uchumi kwa wanabukoba ambapo amelenga kuwasaidia wananchi zaidi ya 2000 kupata ajira.

Anasema, atahakikisha anakuza pato la mwananchi wake ambapo amelenga mwananchi apate pato kutoka sh. 400,000 za sasa hadi kufika 650,000 pamoja na kutengeneza vitega uchumi ambavyo vitamsaidia kufikia hapo na kukuza uchumi kwa kasi ikiwa ni pamoja na wananchi kupata ajira.

"Kwa kufanya hivyo hautakuta vijana wangu na wananchi kwa ujumla wanalanda landa bila kazi yoyote na hilo ndilo ninalosema katika ukuzaji wa uchumi na ajira kwa wanabukoba lakini ajira hizi lazima ziwepo kutokana na kwamba zoezi hilo linaweza kwenda ili kupambana na tatizo la ajira ambalo ni changamoto kubwa, kinacholengwa kufanyika hivi sasa ni kuhamishwa kwa stendi ya Bukoba Mjini na kuipeleka eneo la Kyakailabwa.

Anasema, baada ya kupelekwa kwa stendi hiyo vijana watapata ajira kubwa kutokana na mabasi yatakapokuwa yakifika kutoka katika mikoa mbalimbali watatakiwa kuwabeba kwa kutumia usafiri wa aina mbalimbali wasafiri wanaorudi na kwenda kwenye safari zao.

Anaongeza kuwa katika stendi ya Kyakailabwa biashara nyingi zitakuwa zikifanyika na vijana wengi wataweza kujiajiri kupita kitegauchumi hicho kuliko kuendelea kukaa bila kazi kama hali ilivyo sasa.

Anasema kuwa vile vile katika soko la Kyakailabwa wanategemea kujenga shoplaite kubwa, mzuri na ya kisasa ambayo itatumiwa na wananchi pamoja na Jeshi.

"Jengo litakalojengwa ilipo stendi litakuwa ni kubwa, zuri na litakuwa na vitengo tofauti tofauti vya kufanyia shughuli za uzalishaji lakini pia litatoa hata ajira kwa vijana kwani lazima wasomi na vijana wengine wajishughulishe humo," anasema.

Kwa upande wa elimu anasema kuwa Manispaa imeanzisha Chuo cha Ualimu hivyo vijana wengi wataweza kujiunga katika chuo hicho na siyo kuangaika huko na kule.

"Pia tuna Tawi la Tumaini ambalo tunategemea lianze Septemba, 2012 lakini pia kwa upande wa shule za manispaa hatuna tatizo lolote kwani tumepata ufaulu wa asilimia 83 huku tukiwa na vyumba vya madarasa kwa asilimia 100 hivyo hatuna upungufu wowote" anasema.

"Mimi nimetembea nchi nyingi na nimeona majengo makubwa na mazuri hivyo tunampango wa kujenga soko ambalo ni la kisasa na la kimataifa ambalo kwa hapa Tanzania halipo," anasema Dkt.Amani.

Anatoa wito kwa wazawa wa Mkoa huo kutoukimbia mji huo na kuwataka wafike kwa ajili ya kuwekeza, kujua maendeleo ya mkoa wao.

"Lakini pia si tu wazawa bali tunawakaribisha hata watu wengine kwa ajili ya kuja kuangalia maendeleo yetu hata wale wa nchi jirani kwani kutoka bukoba hadi huko ni kilometa 290 wakati ni karibu sana kutoa bukoba hadi Kigali hivyo waje," .


No comments:

Post a Comment