24 May 2012

Mama kizimbani kwa kujaribu


Na Said Hauni, Lindi

MKAZI wa Kata ya Mtanda Halmashauri ya Lindi Bi. Aluminata Alois Kimisa (38) amefikishwa mahakama ya mkoa huo akikabiliwa na shitaka la kujaribu kumuua mtoto mchanga aliyemzaa.    

Mwanamke huyo alifikishwa mahakamani hapo Mei 22, mwaka huu na kusomewa shitaka lake na Mwanasheria wa Serikali Bw. Juma Maige.    

Akisomewa shitaka lake mbele ya hakimu Bi. Liliani Lugalabamo Bw. Maige alidai Mei 19 mwaka huu mishale ya saa za usiku, mshitakiwa kwa makusudi alijaribu kumuua mtoto wake mchanga kwa kumtumbukiza ndani ya shimo la choo.   

Bw. Maige aliiambia mahakama hiyo iliyokuwa imefurika wasikilizaji kuwa mshitakiwa Aluminata alifanya kitendo hicho huku akifahamu kwamba uamuzi anaoufanya ni kosa kwa mujibu wa sheria.

Mwanasheria huyo alidai kutokana na kitendo hicho, mshitakiwa amefanya kosa chini ya kifungu cha 199 na 380 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya Marejeo ya mwaka 2009.

Aliiomba mahakama hiyo kutompa dhamana mshitakiwa huyo kutokana na kichanga hicho kuendelea kulazwa hospitalini na inadaiwa hali yake siyo mzuri.

Hata hivyo, ombi la mwanasheria huyo lilipingwa na hakimu Bi. Lugalabamo kwa maelezo kwamba dhamana ni haki ya msingi kwa mshitakiwa ikizingatiwa kosa linalomkabili linahusiana na malezi ya mtoto wake mchanga.

Kufuatia kauli hiyo, hakimu huyo amepanga kutoa uamuzi wa kumpatia au kutompatia dhamana mshitakiwa huyo Mei 28, mwaka huu na kuamuru kuendelea kukaa hospitalini chini ya ulinzi wa maofisa wa magereza kwa ajili ya kumpatia kichanga hicho huduma ya kunyonya maziwa ya mama yake.

Mtuhumiwa alitinga mahakamani hapo akiwa amevalia nguo aina ya vitenge huku kichwani akiwa amefunika nywele zake kwa mzura wa rangi ya kahawia akionekana kutokuwa na wasiwasi kwa kosa linalomkabili kwa kujibu kila analoulizwa.

Bi. Aluminata, ambaye huyo ni mtoto wake wa pili kumzaa, inadaiwa alichukua uamuzi wa kumtupa mtoto wake huyo kwenye choo cha Shule ya Msingi Mtanda kwa maelezo ya kukataliwa mimba ya kichanga hicho na mwanaume aliyempa ujauzito.


1 comment:

  1. anyongweeeeeeeeeee coz anatabia mbaya kama angekua n ini yeye angekfika hapo alipo?

    ReplyDelete