23 May 2012
Madiwani Kishapu wamkataa Mkurugenzi
Na Suleiman Abeid, Kishapu
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, wamefikia azimio la pamoja na kumkataa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Bw. Theonas Nyamuhanga.
Mbali ya kumkataa Mkurugenzi huyo ambaye hakuwepo katika kikao hicho, pia walimuomba Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo (OCD), kuhakikisha anamtafuta Bw. Nyamuhanga na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Sambamba na hatua hiyo, madiwani hao pia wameagiza Benki ya NMB, Tawi la Manonga, ishtakiwe kwa kuhusika na upotevu wa fedha za halmashauri sh. bilioni 6.7.
Madiwani hao walifikia uamuzi huo jana katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wakidai kushangazwa kwao na kitendo cha Serikali kushindwa kumchukulia hatua Mkurugenzi huyo.
Kutokana na hali hiyo, madiwani hao wametishia kufunga na kulala nje ya ofisi za Mkurugenzi ili kuhakikisha haingii tena ofisini.
“Ndugu Mwenyekiti, inasikitisha sana, huyu Mkurugenzi leo ni mara ya tatu tumekuwa tukimkataa lakini haondoki,” walisema madiwani hao na kuongeza kuwa, wameguswa na tuhuma mbalimbali zinazomkabili na kama Serikali itashinikiza aendelee na kazi basi, watajiuzulu nyadhifa zao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment