18 May 2012
KIFO CHA MAFISANGO: Mapya yaibuka *Niyonzima aachiwa usia *Kaseja, Maftah,Boban wamwaga chozi
Na Elizabeth Mayemba
KIFO cha kiungo mshambulaji wa Simba raia wa Rwanda Patrick Mutesa Mafisango, kilichotokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 10 alfajiri, mazingira yake yalikuwa ya kusikitisha sana.
Jana vilio vilitawala nyumbani kwa mchezaji huyo huku kila mmoja asiamini kile kilichotokea hasa kwa wachezaji wenzake ambao walishindwa kujizuia na kuangua vilio.
Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo, rafiki wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Olya Ilemba, ambaye alishuhudia kifo cha mchezaji huyo, alisema mauti ilimfika Mafisango wakati wakitokea kujirusha klabu ya Maisha, ambako bendi ya FM Akademia 'Wazee wa Ngwasuma' walikuwa wakipiga siku hiyo.
"Baada ya muziki kumalizika tuliondoka mimi Mafisango na watu wengine watatu, Mafisango ndiye alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Cresta nyeupe, lakini alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi sana, tulipomuuliza akasema kuwa amechoka anahitaji kupumzika hivyo tumuache," alisema Olya.
Alisema walipofika maeneo ya VETA chuo cha ufundi Chang'ombe eneo ambalo unamalizikia ukuta, walikutana na mwendesha guta hivyo Mafisango akajaribu kumkwepa, lakini akiwa katika harakati hizo ghafla ilitokea pikipiki ambayo ilikuwa mwendo wa kasi sana.
Olya anasema wakati Mafisango anajaribu kumkwepa mwendesha Pikipiki bahati mbaya gari iliacha njia na kuparamia mtaro ambapo mbele yake kulikuwa na miti hivyo akaing'oa.
"Kwakweli ile ajali ilikuwa mbaya sana kwani baada ya gari kusimama tulimfuata Mafisango na kumkuta jicho la upande wa kushoto likiwa limechomoka huku akiwa ameumia vibaya kichwani, tukajaribu kuondoa kiwiliwili ambacho kilikuwa kimegandamizwa na usukani," alisema
Baada ya kumtoa hapo anasema kuna rafiki yao mwingine Gaspa Karemera alikuwa amechanganyikiwa baada ya kuhisi kuwa Mafisango amefariki, lakini alimwambia wajikaze ili wampeleke hospitali.
Anasema habati nzuri kuna teksi ilikuwa inapita hivyo wakaisimamisha na kumpakia mpaka hospitali ya taifa ya Muhimbili ambapo baadaye walithibitisha kifo chake.
"Inauma sana dada, Mafisango kipenzi chetu ametuacha wakati bado tunamuhitaji, tena ilikuwa jana (leo) aondoke kwenda kwao Rwanda kujiunga na timu ya taifa ya huko, lakini safari yake imekuwa ni kifo," alisema huku akilia Olya.
Msiba wa Mafisango upo Chang'ombe maduka mawili kwenye nyumba wanayoishi wachezaji wenzake, Gervas Kago raia wa Afrika ya Kati na Mganda Derrick Wallulya, inasemekana nyumba anayoishi marehemu nafasi ni finyu hivyo msiba wakahamishia kwa wenzake.
Taarifa ambazo zimelifikia gazeti hili ni kwamba mwili wa marehemu utaagwa leo kwenye viwanja vya TTC Club Chang'ombe, kuanzia saa nne asubuhi,kabla ya kusafirishwa saa 10 jioni kwenda kwao Rwanda kwa ajili ya taratibu za mazishi.Marehemu ameacha mke na mtoto mmoja wa kiume, Chris Paul, mwenye umri wa miaka mitano
Wakati huo huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji huyo wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango kilichotokea jana alfajiri kwa ajali ya gari Dar es Salaam.
Katika taarifa iliyotolewa na Ofisa habari wa Shirikisho hilo, Boniface Wambura ilieleza kuwa, msiba huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya kazi yake kwa bidii.
"Kifo chake ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto zake zilikuwa dhahiri uwanjani,"ilieleza sehemu ya taarifa.
"TFF inatoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba, Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito na Mungu aiweke roho ya marehemu Mafisango mahali pema peponi. Amina,"iliongeza tarifa hiyo.
Pia kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima alisema kuwa msiba huo ni mzito sana kwa Mnyarwanda mwenzake, kwani jana saa ambayo Mafisango alipata ajali na kufariki ulikuwa muda wa yeye kuondoka kwenda Rwanda kujiunga na timu ya taifa ya Amavubi.
"Lakini cha kushangaza nilipoondoka nyumbani nilisahau tiketi ya ndege, ile na fika uwanja wa ndege nakumbuka kuwa sikubeba tiketi, wakati narudi nyumbani iliingia simu ya kunitaarifu msiba huo, kwakweli sikuamini mpaka pale nilipoenda Muhimbili," alisema Niyonzima.
Alisema kumbe zote hizo zilikuwa ni dalili kwani haikuwahi hata siku moja akasahau tiketi, lakini jana hali hiyo ilimkuta ambapo anasema siku moja kabla ya kifo chake walizungumza sana.
"Hakusita kunikumbusha kuwa, nitunze jezi yake namba 30 ambayo tulibadilishana wakati tulipocheza nao na sisi kufungwa mabao 5-0, aliniambia kuwa jezi hiyo nisiigawe kwa mtu yeyote kwani itakuwa ni kumbukumbu yangu, kumbe jamaa kama alijua anakufa, nitamkumbuka daima,"alisema Niyonzima
Nao wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars' wale wa Simba baada ya kupata taarifa za msiba huo walijikuta wakinyong'onyea na kushindwa kufanya mazoezi kabisa ambayo yalikuwa yakifanyika Uwanja wa Karume chini ya kocha wao mpya Kim Poulsen.
Wachezaji wa Simba Juma Kaseja na Amir Maftah walishindwa kujizuia na hivyo kuangua vilio ambapo walishindwa kabisa kufanya mazoezi, ambapo daktari wa timu hiyo Mwanandi Mwamkemwa alikuwa akifanya kazi ya ziada ya kuwapa maneno ya kuwafariji.
Hata hivyo mazoezi yalipomalizika, wachezaji wote waliruhusiwa kwenda kwenye msiba wa mchezaji mwenzao, huku Boban akiunganisha moja kwa moja Muhimbili ambako ulihifadhiwa mwili wa marehemu.
Mafisango alikuja nchini mwaka juzi na kujiunga na timu ya Azam FC kabla ya kuhamia Simba mwaka jana, alizaliwa Machi 7, mwaka 1987 mjini Kinshasa, DRC alikoanzia soka kabla ya kuhamia Rwanda, ambako baadaye alichukua uraia wa nchi hiyo.
Kabla ya kuja Tanzania aliichezea timu ya APR ya Rwanda na Mechi ya mwisho kuichezea Simba ilikuwa dhidi ya Al Ahly Shandy yaSudan iliyofanyika Jumapili katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penalti 9-8, kufuatia sare ya jumla ya 3-3.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment