04 May 2012

JK ampa ubunge James Mbatia


*Wamo Profesa Muhongo, Bi. Janet Mbene
*Watabiriwa kuwemo kwenyea baraza jipya
*Nchimbi awaomba Watanzania wamuombee
*Tibaijuka, Magufuli nyota zao zang'aa

WAKATI Rais Kikwete anatarajia kufanya mabadiliko katika baraza kake la mawaziri wakati wowote sasa, jana amemteua Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, kuwa mbunge.

Mbali na Bw. Mbatia, Rais Kikwete amemteua Profesa safi Profesa Sospeter Muhongo, Bi. Janet Mbene, kuwa wabunge. Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, ilieleza kuwa Rais Kikwete amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka ya uteuzi aliyopewa.

"Rais Kikwete amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka ya uteuzi aliyo nayo chini ya Ibara ya 66(i) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Uteuzi huo umetafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa watu hao wanaandaliwa kuwa mawaziri, hasa ikizingatiwa kuwa Rais anatarajiwa kufanya mabadiliko ya baraza lake wakati wowote kuanzia sasa.

Profesa Muhongo ambaye ni mtaalam wa masuala ya madini Geology anatabiriwa kukabidhiwa kuongoza Wizara Nishati na Madini, huku nafasi za wengine walioteuliwa zikiwa bado kitendawili.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana Mhadhiri wa Kitivo cha Sayansi za Siasa katika Chuo Kikuu cha SAUT, Profesa Mwesiga Baregu, kuhusu uteuzi huo, alisema; "Anawaandaa kwa ajili ya kuwaweke katika baraza lake la mawaziri."

Profesa Baregu alisema alisema baraza la mawaziri la sasa limepwa ndiyo maana ameamua kuchukua watu kutoka nje ya CCM. Alimshauri Rais Kikwete, kuteua baraza la mawaziri lenye sura mpya na watu wachache na wenye uwezo wa kufanyakazi.

Alitaja sifa nyingine ambazo anataka mawaziri wapya kuwa nazo kuwa ni uaminifu, wawajibikaji, uadilifu na wenye kuleta tija kwa wananchi wanaowatumikia.

"Akichagua wale wale wa zamani hakutakuwa na mabadiliko yoyote," alisema Profesa Baregu. Alishauri mabadiliko hayo ya baraza yafanyike haraka  kwani kuwaacha wanaotuhumiwa kwa kushindwa kuwajibika kuendelea kuwepo ofisini kunaweza kuwapa mwanya wa kupoteza vielelezo pindi watakapofikishwa kwenye vyombo vya sheria.

"Mimi namshauri rais kufanya mabadiliko haraka iwezekanavyo, kwani kuendelea kuwepo ofisini kwa mawaziri hao ni tatizo na mambo yanaweza kuharibika kwa kuwa wana uwezo wa kuchukua vielelezo na kupoteza ushahidi," alisema.

Hata hivyo alisema  kufanya mabadiliko pekee hakutasaidia bali  kinachotakiwa ni kuwatendea haki mawaziri hao kwa kuwafikisha mahakamani ili watakaobainika.

Alisema mbali na kubadilisha baraza la mawaziri, pia anatakiwa kuwachukulia hatua wote waliohusika wakiwemo makatibu wakuu wa wizara kama wanahusika.

Alisema upotevu wa fedha ni matokeo ya kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa mawaziri hao. Alipoulizwa ni mawaziri wapi wanafaa kubaki kwenye safu mpya itakayoundwa, alisema atatoa maoni yake baada ya uteuzi.

Naye, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dkt. Helen Kijo- Bisimba, alisema kubadilisha mawaziri si suluhuhisho kukabiliana na tatizo la viongozi kutowajibika.

Alisema kuwa suluhu ni kuwawajibisha wale wote waliohusika na  kwa kuwfaikisha mahakamani ili haki itendeke.

Kuhusu makatibu wakuu wambao ndio watendaji, Dkt. Kijo-Bisimba alisema kuwa mawaziri hao walitakiwa kuwawajibisha makatibu wakuu pale wanapoona kwamba hawarishishwi na utendani wao wa kazi kwa kuwa wao ndio wapo nafasi za juu kiutendaji.

Mwenyekiti wa Chama cha PPT-Maendeleo, Bw. Peter Mziray, alisema wabunge wamemweka Rais Kikwete kwenye kona mbaya, hivyo ni lazima afanye mabadiliko kwa kuteua mawaziri ambao wananchi wanawaamini.

Pia alishauri baraza atakalounda Rais Kikwete, liwe dogo, kwani la sasa ni kubwa kiasi kwamba inawezaka wakati mwingine akashindwa kuwafahamu.

"Ndiyo maana waziri anaweza kuwa na mali nyingi, lakini akashindwa kufahamu kwa sababu hana muda wa kuwafuatilia," alisema Bw.Mziray.

Aliwataja mawaziri wanaofaa kuwemo kwenye baraza hilo kuwa ni Profesa Anna Tibaijuka, Dkt. John Magufuli, Dkt. David Matayo, Bw. Bernard Membe na Bw. Shamsa Vuai Nahodha.

Wakati huo huo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Emanuel Nchimbi, amewaomba Watanzania kumuombea ili aweze kuteuliwa tena kurudi kwenye baraza la mawaziri.

Alisema bado ana moyo wa kuwatetea Watanzania katika mambo mbalimbali ili kuijenga nchi hii.

"Bado ninahitaji kuwasaidia Watanzania wenzangu na ninawapenda, ndiyo maana leo hii tena muda kama huu ambapo mawaziri wengi wapo katika sala za kumuomba Mungu wao ili waweze kupita tena, lakini mimi nimeamua kuja kwenu kwa ajili ya upendo wangu na ni moja ya kazi yangu,"alisema, Dkt. Nchimbi.

Aliongeza kusema kuwa angeweza kumtuma hata mwakilishi wake ili afike katika hafla ya uzinduzi wa mwongozi wa wamiliki na mameneja wa vyombo vya habari, lakini kwa kuwa anafahamu maana yake, ndiyo maana ameamua kufika mwenyewe.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) Bw. Regnald Mengi alimpongeza Dkt. Nchimbi kwa ujasiri wake wa kufika katika uzinduzi huo wakati mawaziri wengine hadi hivi sasa wapo matumbo joto wakiangaika huku na kule ili majina yao yaweze kupitishwa.

"Nakupongeza Dkt. Nchimbi kwa ushujaa ulioonesha ni mkubwa na mawaziri wengi sasa hivi matumbo joto kwa ajili ya kusikiliza kitakachotokea, tunakuona ni jasiri, "alisema Bw. Mengi.

2 comments:

  1. Aombewe arudi kututumikia au kutimiza mpango wake wa kuwania urais 2015? nani asojua! kawatajirishe masangoma huko ....

    ReplyDelete
  2. Jitihada anazofanya Rais ni nzuri.Na nafikiri vile vile angeomba ushauri kutoka vyama vya mageuzi ili kuunda baraza zuri la mawaziri.Ingawavyo kusema ukweli hawezi kupata mawaziri waadilifu kutoka chama chake cha CCM.Kwa sasa ni bora baraza siyo baraza bora la mawaziri.

    ReplyDelete