11 May 2012
Jengo ofisi ya DC lakosa choo
Na Queen Lema, Arusha
WAFANYAKAZI wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha wamedai afya zao zipo hatarini kutokana na kukosa choo na kusababisha mazingira ya ofisi hiyo kutapakaa maji machafu.
Suala hilo limekuwa likilalamikiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kupatiwa ufumbuzi huku wafanyakazi hao wakiendelea kukumbwa na adha ya harufu mbaya.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa sharti la kutonukuliwa majina yao kwenye vyombo vya habari, walisema adha hiyo imekuwa ikiwakumba zaidi watumishi waliopo chini ya jengo hilo la ofisi ya mkuu wa wilaya.
Mmoja wa watumishi hao alisema watumishi waliopo ghorofa ya juu wamekuwa wakimwaga maji na kusababisha choo cha chini kuzagaa uchafu.
"Kama mnavyoona hii hali inatisha kwani ni muda mrefu choo hiki kimeziba wenzetu wakimwaga maji huko juu, uchafu wote unatoka," alisema mtumishi huyo.
Wafanyakazi hao kutoka idara mbalimbali za serikali katika jengo hilo, walidai kuwa wamekuwa wakipata shida kutokana na kukosa sehemu ya kujisaidia na kulazimika kwenda umbali mrefu kutafuta huduma hiyo ya choo.
Alidai taarifa ya ubovu wa choo hicho walitoa kwa viongozi akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Bw.Raymond Mushi, bila kupatiwa ufumbuzi. Kukosekana kwa huduma ya choo katika jengo hilo kumewakumba watumishi wa idara mbalimbali za Serikali.
Akizungumzia hali hiyo Katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Emi Lyimo, alikiri kupata taarifa juu ya ubovu wa choo hicho, lakini alidai kuwa suala hilo lipo juu yake na tayari taarifa walishazifikisha ofisi kunakohusika.
Alisema hali ya ubovu wa choo hicho ni ya siku nyingi hata Mkuu wa Wilaya anaifahamu.
Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Bw. Everin Itanisa, alipoulizwa kuhusu ubovu wa choo katika jengo hilo alidai kuwa taarifa hizo anazo na kilichokwamisha ukarabati ni ukosefu wa fedha.
Alisema ukarabati wa choo hicho unahitaji gharama kiasi cha sh.milioni 12 na ofisi yake haikuwa na fedha isipokuwa wamepata nusu baada ya kuamua kuchangishana katika idara zote za ofisi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment