24 May 2012

Huduma za uhakika za maji safi bado tatizo



Na Agnes Mwaijega

PAMOJA na Maendeleo yaliyopatikana katika  nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ,bado hazitaweza kufikia lengo la Milenia katika maji mpaka mwaka 2032.

Tanzania  ni miongoni mwa nchi hizo nayo bado inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa huduma za uhakika za maji safi na mazingira bora.


Pia hazitaweza kufikia lengo la milenia la usafi wa mazingira mpaka mwaka 2175 pamoja na la  kidunia la upatikanaji wa maji kwa wote mpaka mwaka 2360.

Hii inatokana na ukweli kwamba katika maeneo mengi watu bado hawana uhakika wa maji safi,salama pamoja na mazingira bora kwa ustawi wa jamii.

Mpango wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa  (UNDP) unakadiria kuwa upungufu wa upatikanaji wa maji na huduma za Usafi wa Mazingira unazigharimu serikali za nchi hizo asilimia 5 ya pato la jumla kila mwaka ambapo ni sawa na dola bilioni 56.6.

Jambo ambalo ni hatari kwa uchumi wa nchi hizi hivyo serikali zinapaswa kulitafutia ufumbuzi ili fedha hizo ziweze kutumika katika kuendeleza miradi mingine ya maendeleo.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la kimataifa la WaterAid inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 600 kusini mwa jangwa la Sahara  hawapati huduma ya uhakika ya Usafi wa mazingira, wakati watu milioni 335 hawapati maji Safi na salama.

Kutokana na hali hiyo zaidi ya robo tatu ya watoto milioni wa bara la Afrika wanakufa kila mwaka kutokana na maradhi ya kuhara ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na ukosefu wa maji safi, salama pamoja na uduni wa huduma za usafi wa mazingira.

Shirika la kimataifa la WaterAid linasisitiza kuwa huduma hizo za muhimu zinapaswa kupewa kipaumbele na serikali.

Linatoa wito kwa serikali za Kiafrika kujitoa katika kupeleka huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa wananchi wake.

Meneja wa Programu ya Pan- Afrika, Shirika la WaterAid Bw. Nelson Gomondo anasema
nchi za Kiafrika zina hatari ya kukosa kuaminika kama hazitatumia fursa zilizopo katika kupambana na  changamoto hiyo kwa kuongeza kasi katika kuhakikisha kuwa upatikanaji wa maji na huduma za usafi wa mazingira  katika nchi zao unakuwa wa uhakika.

Ikiwa maelfu ya watoto wanakufa kila siku,na  serikali hizi zinashuhudia vifo ambavyo vinasababishwa na ukosefu wa maji salama  lazima zirejee ahadi zao za kuongeza uwekezaji kwenye Usafi wa mazingira.

Ahadi zilizokwisha wekwa na Serikali hizi za Kiafrika ni  pamoja na zile zilizowekwa hivi karibuni na nchi 30 za kiafrika katika Mkutano wa viongozi serikali hizo uliofanyika mjini Washington.

Katika mkutano wa mwaka 2007 uliohusisha nchi hizo ziliweka Azimio ambapo serikali zilikubaliana  kuwekeza 0.5% ya bajeti ya pato lake la mwaka kwenye usafi wa mazingira na ule wa Sharm El-Sheikh mwaka 2008 ambapo walikubaliana  kuongeza kasi ya kufikia malengo ya maji na usafi wa mazingira.

Karibu nchi 30 za Kiafrika na serikali za nchi nyingine duniani walikubaliana kujitahidi utekelezwaji wa ahadi ya kuongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 5% na Usafi wa Mazingira 7% katika nchi zao.

Serikali ya Tanzania iliahidi kuwa kufikia mwaka 2015, watu zaidi milioni 27  watapata huduma za usafi wa mazingira na milioni 4.2 zaidi kupata maji safi na salama.

Hata hivyo kwa hali ilivyo katika maeneo mengi ambapo Watanzania wengi wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na uhakika wa huduma ni wazi kwamba malengo hayo hayatafikiwa.

WaterAid pia ilifanikiwa kushinikiza malengo  hayo kutekelezwa katika uongezaji wa kasi ya  upatikanaji wa huduma hizi muhimu katika mkutano wa  uliofanyika mjini Washingtoni kuhusu Usafi wa Mazingira na Maji kwa kwa wote Aprili mwaka huu.

Hata hivyo mpaka sasa ni Serikali moja tu ya Sao Taome na Principal ndio zilizotimiza malengo ya maazimio katika mkutano huo.

Mwakilishi wa shirika la WaterAid Tanzania Bw. Paul Obura,anaongeza kuwa lazima serikali hizo zitafute mbinu nzuri zaidi na kuongeza kasi katika upatikanaji wa huduma hizo.

"Watu hawapaswi kuendelea kuishi katika mazingira ya aina hii ambayo yanaashiria hatari kubwa kwa miaka ijayao," anasema.

Anasisitiza kuwa watunga sera wanapaswa   kubadilishana mawazo ,ujuzi , uzoefu na njia bora zinazoweza kuwasaidia katika kutimiza upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira .

WaterAid inazitaka Serikali za Kiafrika kuchukua hatua kali katika kuhakikisha kunakuwa na  upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa kwa watu milioni 42.8 na kuongeza upatikanaji wa huduma ya Usafi wa Mazingira kwa watu milioni 42.9 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Pia katika maeneo ya vyanzo vya maji Watanzania wanapaswa kuzingatia usafi wa mazingira na kutunza maji.

Hatua hii itakuwa nzuri na itasaidia nchi hizo kufikia malengo yake.





No comments:

Post a Comment