14 May 2012
Good Hope kuibua makocha, Waamuzi Songea
Na Mhaiki Andrew, Songea
SHIRIKA lisilokuwa la Kiserikali la Klabu ya michezo ya Good Hope la mkoani Ruvuma, lina mpango na mikakati ya kutoa mafunzo ya ukocha na waamuzi kwa wanafunzi wa shule za Sekondari ikiwa na lengo la kuibua na kuendeleza taaluma ya michezo mkoani hapa.
Akizungumza mjini hapa juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Joseph Mapunda alisema mafunzo hayo yatalenga wanafunzi wa shule hizo za Sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu katika kuwapa taaluma ya michezo badala ya kutegemea makocha kutoka nje ya mkoa kuja kufundisha.
Alisema Shirika hilo limejiwekea malengo endelevu katika kusaidia kuinua michezo hiyo kitaaluma ambapo alidai baada ya kukamilika zoezi hilo kwa shule za Sekondari pia mafunzo hayo yatatolewa kwa vijana wa shule za msingi kwa kuanzia darasa la tano.
Alisema kabla ya kuanza kwa utoaji wa mafunzo ya ukocha kwa wanafunzi hao, alidai bodi ya Shirika hilo limekutana na kuweka mikakati itakayowezesha kufanikisha zoezi hilo.
Alisema katika mapendekezo yao wamedai wataanzia na shule za Sekondari katika wilaya mbili za Songea na Namtumbo na baadaye Nyasa, Mbinga na Tunduru.
Aliongeza mafunzo hayo yatatolewa kwa michezo 10 ambayo baadhi ni soka, netiboli, ngumi, riadha na mpira wa wavu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment