11 May 2012

DC ahamasisha matumizi bidhaa zenye ubora


Na Jovin Mihambi, Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Evarist Ndikillo, amewataka wafanyabiashara nchini kuagiza bidhaa kutoka nchi za nje zenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa na vinavyoendana na uchumi wa nchi ili kila mwananchi aweze kumudu kuvinunua na vitumike kwa muda mrefu.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bw. Saidi Amanzi, katika hotuba yake aliyoitoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wakati wa ufunguzi wa duka la kuuza pikipiki na bidhaa zingine zinazotengenezwa na kampuni ya Honda ambalo limefunguliwa na Kampuni ya QM Quality Motors Limited lenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara nchini wamekuwa wakiingiza bidhaa mbalimbali ambazo hazina ubora na nyingi kutoka China.

Alisema kufunguliwa kwa duka hilo la kuuza pikipiki za Honda pamoja na bidhaa zingine ambazo ni jenereta, pampu za kusukumia maji, injini za kuendeshea mitumbwi limekuwa ni mkombozi kwa wananchi wa kanda ya Ziwa na mikoa mingine ya jirani.

Naye Meneja mauzo na Masoko wa kampuni ya QM Quality Motors Limited, Bw.Sudhir Borgaonkar, alisema bidhaa za kampuni yake ikiwemo pikipiki za Honda ambazo alisema zinauzwa bei nafuu ikilinganishwa na zile za kutoka China.

No comments:

Post a Comment