09 May 2012

Albino waombewa elimu serikalini



Na David John, Aliyekuwa Lindi

MKURUGENZI wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Under The Same Sun Bi. Vick Ntetema ameitaka Serikali kuwajengea mazingira mazuri hususan elimu walemavu wa ngozi ili kuweza kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo katika nyanja hiyo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki mkoani Lindi katika maadhimisho ya siku ya Walemavu wa Ngozi Bi. Ntetema alisema walemavu wa ngozi wanakabiliwa na changamoto nyingi hasa katika upande wa nyanja ya elimu hivyo ni vema serikali wakaangalia namna ya kuweza kuwaboreshea mazingira.

"Kuna changamoto nyingi ambazo ALBINO wanakumbuna nazo ikiwa pamoja na kukosekana wa vifaa maalumu vya kukabiliana na masomo hasa wakiwa darasani"alisema Bi, Ntetema.

Alisema walemavu hao wangozi wanahitaji mazingira mazuri ya kupata elimu ikiwa pamoja na kuwapatia mahitaji muhimu kama vile Miwani yakuonea , Kofia , Nguo zakufunika Miili yao, pamoja na Lotioni yakujipaka katika mwili.

Alisema, imebainika zaidi ya asilimia 60 ya walemavu wa ngozi hawana ajira huku wengi wao wakiwa hawana elimu ya kutosha hivyo ifikie mahali kuwajengea uwezo wa elimu waweze kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kupata ajira baada ya masomo.

Katika hatua nyingine Bi. Ntetema aliitaka serikali kuangalia upya mitaala ya elimu ili iweze kuwa chachu pia kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kufanya vizuri na hasa katika kupunguza viwango vya ufaulu kwa Albino ikiwa pamoja na kuongeza muda pindi wanapokuwa kwenye kipindi cha mitihani.

"Kuna matatizo makubwa katika mitaala ya elimu tumeanda mapendekezo ambayo tumekwisha yapeleka Wizara ya Elimu ili kurekebisha baadhi ya maeneo, kutoa fursa kwa Albino kuweza kupata elimu ya sekondari kwa wingi zaidi tofauti na ilivyo sasa," alisema.



No comments:

Post a Comment