11 May 2012

Abiria kununua tiketi kwa simu


Darlin Said na Radhia Adam

KAMPUNI ya Mobile Ticketing LTD imezindua huduma mpya ya kukata tiketi za usafiri wa mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani inayojulikana kwa jina la "Tiketi popote" kwa kutumia simu za mikononi ambapo mteja atapata huduma ya tiketi popote alipo.

Huduma hiyo inategemewa kutumika kwa mikoa yote ya Tanzania ambapo kwa sasa huduma hiyo itaanza kutolewa katika mikoa ya Dar es Salaam,  Mwanza, Arusha, Tabora, Mtwara, Kilimanjaro, Lindi, Morogoro pamoja na nchi za jirani.

Huduma hiyo imeanza kutumika rasmi mara baada ya kuzinduliwa na kwa sasa inahusisha huduma za M-pesa, Airtel money pamoja na Easypesa.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw.Abert Muchuruza, alisema wameanzisha kampuni hiyo kwa lengo la kuondoa usumbufu wanaoupata wasafiri pindi wanapoenda kukata tiketi ikiwemo kuuziwa tiketi bandia, kuzidishiwa nauli na wapiga debe na kuuziwa tiketi za magari yasiyo safiri.

Huduma hiyo inatoa taarifa zote za mteja ikiwemo namba ya gari, namba ya siti pamoja na jina la gari atakalosafiri nalo abiria na ikitokea tatizo, msafiri anajulishwa.

Mbali na huduma ya tiketi kwa mabasi kampuni inatarajia kutoa huduma kwa vyombo vingine vya usafiri kama treni na meli.

No comments:

Post a Comment