12 April 2012

Yanga waenda Kanda ya Ziwa

*Sendeu alalamikia ratiba ya ligi
Na Elizabeth Mayemba
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wameondoka Dar es Salaam jana kwenda Kahama mkoani Shinyanga kwa ajili ya mechi ya ligi hiyo itakayopigwa Jumapili dhidi ya Toto African ya Mwanza.

Leo timu hiyo inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Kahama Ambassador, ambapo kesho wataanza safari kwenda jijini Mwanza.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema kikosi chake kiliondoka jana asubuhi kwa ajili ya mechi hiyo, ikiwa na leo kujipima nguvu na Kahama Ambassador.

"Timu yetu imeondoka leo (jana), kwa ajili ya mchezo wetu na Toto Jumapili, hivyo tumeona ni vyema kama tukicheza mchezo wa kirafiki leo kabla ya kwenda Kahama," alisema Sendeu.

Alisema baada ya mechi ya Jumapili dhidi ya Toto, timu hiyo itaondoka siku inayofuata kwenda Bukoba ambako Jumatato ijayo watacheza na Kagera Sugar, baada ya hapo watarejea Dar es Salaam.

Sendeu alisema wakiwa Dar es Salaam, Jumapili ijayo watacheza na Polisi Dodoma, baada ya hapo wataondoka tena kwenda jijini Arusha kucheza na JKT Oljoro.

Hata hivyo Sendeu amelalamikia ratiba ya mechi hizo za ligi imewabana mno, hivyo timu yao itashindwa kufanya mazoezi kwa kuwa muda mwingi watakuwa safarini.

"Kwa kweli ratiba zimetubana sana, hivyo timu yetu itakosa hata muda wa kufanya mazoezi kwa kuwa muda mwingi tutakuwa barabarani, hii ni hatari sana hasa kwa mechi zetu hizi za mwisho," alisema.

No comments:

Post a Comment