Na Livinus Feruzi, Kagera
SHIRIKA la Kuwezesha Watoto Yatima na Wajane katika Manispaa ya Bukoba la Matumaini Mapya linatarajia kutoa ruzuku ya zaidi ya sh. milioni 48.4 kwa wanawake wajane na walezi wa watoto yatima 200 lengo likiwa ni kuwapunguzia ugumu wa maisha unaowakabili.
Mratibu wa shirika hilo Bw.
Gosbert Kaserwa alisema hayo
jana wakati akifungua mafunzo ya
siku tano kwa akinamama wajane
na walezi wa watoto yatima 40 wa
awamu ya kwanza kutoka wilaya za
Bukoba na Missenyi.
Alisema kabla ya wanawake
hao kupatiwa ruzuku hiyo kwanza
shirika linawapatia mafunzo juu ya
masuala mbalimbali ili kuwajengea
uwezo wa kusimamia na kutetea
haki zao ambapo zaidi ya shilingi
milioni 66 zitatumika katika
mafunzo hayo.
Bw. Kaserwa alisema shughuli
hiyo ya utoaji wa ruzuku ambayo
itaenda sambamba na mafunzo
itafanyika kwa awamu tano tofauti
huku kila mwanamke akitarajiwa
kupewa kiasi cha sh. 240,000.
Mratibu huyo aliwataka
wanawake hao kutumia fedha
hizo za ruzuku katika kuendeleza
miradi yao ili ziwasaidie kuboresha
maisha yao na familia zao ikiwemo
kupata mahitaji muhimu ya kila
siku ambayo awali walikuwa
wanashindwa kuyapata.
"Baada ya ruzuku shirika linataka
kuona akinamama wajane ambao
walikuwa wanakula mlo mmoja,
waliokuwa wanashindwa kupata
matibabu hospitali pale wanapougua
au kupeleka watoto shule kwa
sababu ya ugumu wa maisha tukija
kufanya tathmini tunataka hali iwe
tofauti," alisema Bw. Kaserwa.
“Naomba nitumie nafasi hii
kuwaomba ndugu zangu kwamba
kama unajua hauwezi kutumia
ruzuku kuendeleza miradi na
kukuboreshea maisha useme, maana
baada ya hapa tunataka familia
iwe na uwezo wa kupata mahitaji
muhimu," aliongeza.
Wakati wa mafunzo hayo
ya siku tano mada zipatazo 20
zitafundishwa kwa wanawake hao
ambazo miongoni mwake ni Sheria
ya Ndoa ya mwaka 1971, haki za
wajane na watoto yatima, matumizi
bora ya rasilimali za familia, andiko
la mradi wa kijamii na ukatili na
unyanyasaji wa kijinsia.
No comments:
Post a Comment