03 April 2012

TIC yatoa changamoto kwa wajasiriamali kuhusu elimu

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimetoa changamoto kwa wajasiriamali wadogo na wa kati nchini kusaka maarifa na elimu kama njia ya kujiendeleza kibiashara na kufikia mafanikio.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw. Raymond Mbilinyi ametoa changamoto hiyo mwishoni mwa wiki Mkoani Kilimanjaro muda mfupi mara baada ya kufunga mafunzo ya wajasiriamali wadogo na wa kati zaidi ya thelethini kutoka katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

“Mafunzo kama haya ni muhimu katika ufanyaji biashara katika maeneo yao, hivyo kwa kuliona hilo tutaendelea kuwapa nguvu katika kutoa semina hizi mara kwa mara nafasi inapopatikana,” alisema Mbilinyi.

Aliongeza kuwa kwa sasa wataendelea kujikita kutoa mafunzo haya katika kanda, hasa baada ya kumaliza katika kanda ya Dar es Salaam ambayo ameitaja kuwa ina wajasiriamali pamoja na wawekezaji wengi zaidi kuliko mkoa mwingine hapa nchini.

“Tumeanza mafunzo haya toka mwaka 2009, ambapo jumla ya wajasiriamali wapatao 250 wamepatiwa mafunzo na mafanikio yake yameonekana na tayari tumeshapata mrejesho wa kutosha kutoka kwa wafanyabiashara wenyewe,” alisisitiza.

Alisisitiza kuwa wamekuwa na kawaida ya kuwatembelea wajasiriamali hao katika maeneo yao ya biashara mara tu wanapopewa mafunzo ya aina hiyo ili kuona ni jinsi gani wanaweza kufanya kile ambacho wamepatiwa na wakufunzi wakati wanajifunza.

“Tumekuwa na ziara za mara kwa mara za kuwatembelea watu wetu ili kuangalia na kuona maendeleo yao katika sehemu zao za kazi kama wanasogea mbele hatua moja au bado wako palepale, lakini kwetu sisi tumegundua kuwa maendeleo ni makubwa sana kutokana na aina ya mafunzo wanayopewa na TIC,” aliongeza Mbilinyi.

Alisema Kituo hicho kinafarijika kutoka na kukua kwa biashara, kuongezeka kwa ufanisi na bidhaa kuwa na viwango vya juu kutoka na mafunzo yanayotolewa na kituo hicho.

Tunapenda kulishukuru shirika la Maendeleo la Biashara Duniani la Umoja Mataifa pamoja na Sido ambao tumekuwa tukishirikiana nao kwa karibu wakati wa utoaji wa mafunzo haya, wao wamekuwa chachu ya mafanikio kwa wajasiriamali hawa katika kupiga hatua kubwa kuelekea kuwa wawekezaji wakubwa hapo baadae”. Alisema Mbilinyi.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo mara kwa mara, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema yanaumuhimu mkubwa sana kwa TIC pamoja na kwa wajasiriamali wenyewe kwasababu lengo kuu ni kuwaunganisha wajasiriamali wadogo na wakati ili kufanya biashara na wawekezaji wakubwa wakiwepo wale wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wao baadhi ya wshiriki wa mafunzo hayo, Theresia Ruteta na Clemence Molel wamesema mafunzo hayo ni muhimu sana na wamekiomba kituo cha uwekezaji nchini tic kuendelea kuwainua wajasiriamali wadogo na wakati kwa kuwajengea uwezo hasa kwa kuwapa mafunzo aya aina hiyo ili waweze kukuza mitaji yao ya biashara.

“Sisi tunaamini elimu pekee ndio itakayo mkomboa mtanzania yeyote katika kuondokana na umasikini, kwa ni ukimpa mtu elimu ya ujasiriamali na akajawa na ujasiri wa kufanya biashara ama kazi yeyote aliyonayo ataweza kupiga hatua moja mbele na kukuza uchumi wake” Walisema wajasiriamali hao.

Mafunzo hayo ya siku sita ya kuwajengea uwezo wajasiriamali wa wadogo na wakati ili kuwaunganisha na wawekezaji wakubwa imeandaliwa na  Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC)  kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Biashara Duniani la Umoja wa Mataifa (UNCTAD).

No comments:

Post a Comment