16 April 2012

Simba yaendelea kujikita kileleni

Na Elizabeth Mayemba
VINARA wa Ligi Kuu Simba, jana waliendeleza ubabe katika mechi za ligi hiyo baada ya kuinyuka Maafande wa Ruvu Shooting bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao la Simba lilifungwa dakika ya 80 kupitia kwa Patrick Mafisango ambaye alipokea pasi ya Haruna Moshi 'Boban'.

Kwa ushindi huo Simba imeendelea kujikita kileleni mwa ligi hiyo ikiwa na pointi 53, ikifuatiwa na Azam FC ambayo imefikisha pointi 50.

Simba ilianza kwa kishindo mechi hiyo, ambapo dakika ya saba Salum Machaku akwa na kipa wa Ruvu alishindwa kuiandikia bao timu yake baada ya kuchelewa kupiga shuti na kuwahiwa.

Dakika ya saba Simba ilikosa bao lingine kupitia kwa mshambuliaji wake Gervas Kago ambaye kabla ya kupasiwa Boban Na Victor Costa 'Nyumba' waligongeana na vyema lakini, Kago akashindwa kutumbukiza mpira kimiani.

Baada ya kosa kosa hizo, Ruvu Shooting ilizinduka dakika ya 18 Mohamed Kijuso akiwa na kipa Juma Kaseja alishindwa kutumbukiza kimiani baada ya kuwahiwa na Costa.

Kipindi cha pili Ruvu Shooting walionekana kuimarika na dakika 48, Abdallah Juma ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Kijuso alishindwa kufunga akiwa na wavu huku kipa Kaseja akiwa ametoka golini.

Katika kipindi hicho Simba iliwatoa Kago na Machaku na kuwaingiza Uhuru Selemani na Edward Christopher.

Dakika ya 78 Mafisango alikosa bao la wazi baada ya kupasiwa pasi murua na Uhuru Selemani, lakini hata hivyo badala ya kufunga akapaisha mpira juu.


No comments:

Post a Comment