03 April 2012

Msitumie kampuni zinazowanyonya wakulima-Dkt Mahenge

Na Rashid Mkwinda, Makete
MWENYEKITI wa Bodi ya Pareto Dkt. Binilith Mahenge amewataka watendaji wa wilaya hiyo mkoani Njombe kutotumiwa na baadhi ya kampuni ambazo zina  nia ya kuwanyonya wakulima wa zao la pareto kwa kununua kwa bei ya chini.
Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani mwishoni mwa juma Dkt. Mahenge ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Makete alisema kuwa, Wilaya ya Makete inategemea zao  la Pareto likiwa ni moja kati ya mazao ya kibiashara hivyo, wakulima wanatakiwa kupewa fursa ya kuuza bidhaa zao kwa uhuru bila shinikizo.

Alisema kuwa awali wakulima wa pareto walikuwa na matatizo ya soko na hivyo  kulazimika kuiuzia pareto kampuni moja ambayo nayo ilikuwa inanunua pareto kwa bei ya chini na kwamba kwa kuwa yamejitokeza kampuni nyingine ambayo yananunua kwa bei ya juu yaachwe yapambane ili wakulima wanufaike.

‘’Kampuni zote zilizopewa  leseni ya kununua pareto yanatakiwa kuingia katika soko, yanatakiwa kukutana na viongozi wa Halmashauri ili kupangiwa maeneo ya kununua ili yasigongane, kampuni zikiwa nyingi mkulima ananufaika,’’alisema Dkt. Mahenge.

Dkt. Mahenge alisisitiza kuwa kumekuwepo na malalamiko ya watendaji na viongozi wa serikali kukumbatia kampuni moja kwa manufaa yao binafsi jambo ambalo linachangia kuwaumiza wakulima na kuwepo dalili za rushwa na kupewa zawadi.

‘’Hivi vijizawadi mnavyopokea mnapaswa kuelewa kuwa vinachangia kuwakandamiza wakulima, kampuni zinatakiwa  kupambana katika ununuzi bila kupendelea kampuni moja," alisema.

Dkt. Mahenge alisema kuwa kampuni zote ziliyopata leseni za ununuzi yana haki sawa na kuwa hakuna kampuni yenye mamlaka ya kuhodhi ununuzi kwa kisingizio cha kutoa mbegu za pareto kwa kuwa mbegu hizo zinatolewa na Bodi ya Pareto nchini.

Kwa upande wao madiwani kutoka kata 21 za Halmashauri hiyo walikubaliana kwa pamoja kuruhusiwa kwa makampuni mengi kununua pareto kwa wakulima kwa kufuata utaratibu utakaopangwa na Halmashauri ya wilaya.

Hivi karibuni kumekuwa na madai ya mgongano baina ya kampuni ya ununuzi wa pareto na Halmashauri ya Wilaya ya Makete ambapo halmashauri indaiwa kuyazuia  baadhi ya kampuni  kununua pareto wilayani humo na kuruhusu kampuni moja

No comments:

Post a Comment