04 April 2012

Majibu kipimo cha mbunge wa CHADEMA hadharani

*Watano washikiliwa kuhusika na vurugu
Na Zourha Malisa

MBUNGE wa Jimbo la Ilemela, mkoani Mwanza, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Highness Kiwia, ambaye alijeruhiwa vibaya kichwani katika vurugu kubwa zilizotokea jijini humo hivi karibuni, amefanyiwa kipimo cha MRI ambapo majibu yameonesha hajapata athari zozote kwenye ubongo.

Habari za kuaminika ambazo zimelifikia gazeti hili, zimesema Bw. Kiwia alifanyiwa kipimo hicho jana mchana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Matokeo ya kipimo yametoka leo mchana na kuonesha kuwa, Bw. Kiwia hajaathirika katika ubongo, hivi sasa anasubiri kufanyiwa kipimo kingine kesho asubuhi (leo),” kilisema chanzo chetu.

Mwandishi wetu alifika hospitalini hapo na kukuta Bw. Kiwia anaendelea vizuri ambapo mmoja wa wauguzi alithibitisha afya ya mbunge huyo kuimarika wakati akisubiri majibu wa kipimo hicho.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Bw. Kiwia alisema hivi sasa anapata maumivu ya kichwa hivyo bado ataendelea kubaki hospitalini hapo kwa matibabu zaidi.

Kwa upande wake, mbunge wa Ukerewe, Bw. Salvatory Naruyaga, hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri na ilitarajiwa kupewa ruhusa ya kurudi nyumbani kati ya jana au leo.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu juu ya hatua ambazo watachukua dhidi ya Jeshi la Polisi ambalo wanalituhumu kwa kushindwa kuwapa msaada, alisema kwa sasa wanaangalia afya zao.

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu Daud Magesa anaripoti kutoka jijini Mwanza kuwa, Jeshi la Polisi jijini humo limeibuka na kauli tata inayopingana na taarifa ya awali juu ya kundi linalodaiwa kuwajeruhi wabunge hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi
mkoani hapa, Liberatus Barlow, alisema jeshi hilo linawashikilia watu 15 ambao wanatuhumiwa kuhusika na tukio la kuwapiga na kuwajeruhi wabunge na mawakala wao.

Alisema wabunge hao walivamiwa na kushambuliwa na wananchi wenye hasira, Aprili Mosi mwaka huu, saa 6:50 katika eneo la Ibanda Kirumba wakiwa katika harakati za kuwasambaza kwenye vituo mawakala wa chama hicho kwa ajili ya kusimamia mchakato wa upigaji kura ili kumchagua diwani wa Kata ya Kirumba.

Kauli ya Kamanda Barlow, ilitofautiana na ile aliyotoa siku ya tukio
kuwa watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa CCM wanadaiwa kuwavamia na kuwajeruhi wabunge hao kwa kuwashambilia kwa
kuwaka mapanga.

4 comments:

  1. kauli tata ya kanda wa polisi mkoani mwanza Bw. Liberatus Barlow inaonesha haeleweki; Lakini Jeshi lake chini ya usimamizi wake ndilo limesababisha uharamia huo. achukuliwe hatua ya kuvuliwa cheo na kushitakiwa.

    ReplyDelete
  2. One of the indicators that govt. is now unable to protect the citizens. If they cannot protect MPs who else they can the plunders!

    ReplyDelete
  3. Nachelea kusema Nchi ilishapoteza mwelekeo zamani kuanzia katika nyanja za uchumi,elimu na afya na sasa kiusalama hasa usalama wa raia.Hali ni mbaya na wananchi tusiposema basi hali itazidi kuwa mbaya kila kukicha.Hivi ninavyozungumza 1Tshs ni sawa na 0.0005 euro.Hii ni aibu kwa nchi yenye rasilimali tele kama Tanzania.Something is wrong.

    ReplyDelete
  4. Mh. Afande Liberatus Barlow, sema ukweli: angepigwa Mbunge wa CCM au kiongozi wa juu wa serikali Jiji la Mwanza lingekuwa limejaa maaskari hata kutoka vyuo vya polisi. Usiku wa tukio Jiji lingalikuwa limesafishwa pamoja na vipigo kwa wingi. wahusika wangekywa wamepatikana usiku huhuo huo hata ingebidi JWTZ lingitumika. Kama wahalifu hao wangehusishwa na chama kama cha CHADEMA, mahabusu ya Jiji yangalikuwa yamejaa.

    JESHI LENU LITENDE HAKI NA LIMWOGOPE MUNGU. KOMESHHENI VITENDO KAMA HIVI MAPEMA AU VTALETA MAMBO MABAYA. MACHO YA WANANCHI YANAONA KAMA HAKI INATENDEKA AU HAITENDEKI.

    ReplyDelete