16 March 2012

Mwenye hoja za maendeleo Arumeru Mashariki ni yake

Na Pamela Mollel, Arusha
KAMPENI za kuwania Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Aprili Mosi mwaka huu zimeanza rasmi ambapo baadhi ya vyama vimezindua kampeni zake kwa mbwembwe huku kila chama kikizidua kwa staili yake, Majira limebaini.

Hata hivyo kupitia tathimini ambayo ilifanywa na gazeti hili limebainisha kuwa vyama vinane vimejitokeza kuwasimamisha wagombea wao katika kinyang'anyiro cha kulitwaa jimbo hilo.

Vyama hivyo ni pamoja na TLP, SAU, NLD, UPDP, NRA na DP ambavyo vimeonekana kuingia katika kinyanganyiro hicho huku Chama cha Mapinduzi (CCM)kikionekana kuchuana vikali na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)

"Shamrashamra kibao zilianza mapema katika mji mdogo wa Usa River huku magari, pikipiki zikiwa zimefungwa bendera ya chama hicho hali iliyopelekea maandamano makubwa...ni furaha lakini tumeanza kujifunza namna ya kuitumia kura yetu," alisema Bw. Julius Soori miongoni mwa wananchi ambao wanatarajia kupiga kura.

Anasema, Chama cha Demokrasia na Maendeleo ndicho kilikuwa cha kwanza kuzindua kampeni zake ambapo katika uzinduzi huo walitumia helkopta ambayo ilikuwa ikizunguka angani "huku wananchi wakijitokeza kushangaa ndenge hiyo ikiwa angani".

Mbali na manjonjo hayo pia katika uzinduzi huo uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Leganga mjini Usa River, gazeti hili lilishuhudia kulikuwepo na farasi ambaye alikuwa akipitapita huku kukiwepo mtu juu ya farasi huyo akiwa amebeba picha ya mgombea Ubunge kwa tiketi ya CHADEMA, Bw.Joshua Nasari.

Katika kampeni hizo pia maandamano makubwa ya watu pamoja na magari bila kusahau pikipiki zilichukua nafasi kubwa katika uzinduzi huo ambao ulikuwa wa aina yake huku wanachama wa chama hicho wakionekana kusisimkwa zaidi.

Hata hivyo kampeni za CHADEMA zilizinduliwa na Mwenyekiti wao Taifa, Bw. Freeman Mbowe wiki iliyopita huku chama tawala CCM kampeni zake zikizinduliwa na Rais Mstaafu, Bw. Benjamini Mkapa katika eneo la Ngarasero Wilayani humo, huku akisindikizwa na wasanii wa kikundi cha vichekesho cha Komedi na Kikundi cha TOT.

Shamrashamra za CCM zilianza asubuhi kwa magari na pikipiki zilizopambwa kwa bendera za kijani na njano ikipita katika mitaa mbalimbali ya Usa River zikiwahamasisha wakazi wa eneo hilo kuhudhuria uzinduzi huo.

Gazeti hili lilishuhudia katika uzinduzi huo CCM ilipata fursa ya kuwapandisha jukwaani wapinzani wa, Bw. Siyoi Sumari kwenye kura za maoni ambapo, Bi. Elishilia Kaaya, Bw. Elirehema Kaaya na Bw. Wiliam Sarakikya walidhihirishia umma kumuunga mkono mgombea Ubunge kwa tiketi ya CCM Bw.Siyoi Sumari.

Hata hivyo, Bw. Pius Msekwa ambaye ni Makamu Mwenyekiti CCM Tanzania Bara aliwaomba Wanaarumeru Mashariki kulinda mila na desturi iliyojengeka ndani ya Taifa na kuwasii wananchi waliofika katika uzinduzi huo kumchagua, Bw. Siyoi kuendeleza jimbo hilo baada ya kifo cha baba yake mzazi marehemu Sumari kilichotokea Januari 19, mwaka huu.

Mgombea Ubunge kwa tiketi ya CCM, Bw. Siyoi Sumari alisema, endapo ataibuka kidedea katika uchaguzi mdogo atahakikisha ahadi zote zilizoachwa na baba yake zinakamilika sanjari na kushughulikia matatizo ya maji na ajira kwa vijana katika jimbo hilo.

Wakati kampeni hizo zikiendelea tayari Chadema wanajigamba kunyakuwa jimbo hilo kiulaini huku Kampeni Meneja CCM, ambaye ni Katibu wa Fedha na Uchumi Bw. Mwigulu Mchemba akisema CCM ina uhakika wa kushinda katika uchaguzi huo kwa kuwa mgombea wao anakubalika.

Pia wakati tathimini hii ya uchaguzi wa Arumeru Mashariki ikiendelea na ukusanyaji wa takwimu mbalimbali kabla ya uchaguzi, juzi Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Bw. Agustino Mrema alizindua kampeni za chama hicho kwa staili yake wakati wa uzinduzi hakuweza kuwasili na mgombea badala yake yeye na wanachama waliendelea na uchaguzi.

No comments:

Post a Comment