23 February 2012
Stars, DRC kimbembe leo Uwanja wa Taifa
Na Zahoro Mlanzi
Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi Taifa Stars, itakayopigwa leo katika huo. (Picha na Michael Machellah)
TIMU ya taifa (Taifa Stars), leo inashuka dimbani kuumana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayopigwa kuanzia saa 10.30 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ni maalumu kwa ajili ya maandalizi kwa timu zote, kujiandaa na mechi za awali za mchujo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani, zitakazofanyika Afrika Kusini.
Hiyo ni safari nyingine kwa Taifa Stars, ambayo ina muda mrefu haijashiriki michuano hiyo mikubwa ya Afrika, kwani katika fainali za mwaka huu zilizofanyikia Equatorial Guinea na Gabon na Zambia kuibuka mabingwa, ilishindwa kufuzu baada ya kuondolewa katika hatua ya makundi.
Taifa Stars imeshindwa kufuzu kwa fainali hizo, ambazo mara ya mwisho ilishiriki mwaka 1980 kwa kufungwa na timu ya taifa ya Morocco kwa mabao 3-2 na kuzima ndoto za Watanzania ambao baadhi yao walikuwa na matumaini kama timu yao ingeweza kuifunga Morocco.
Timu hiyo ilikuwa Kundi D, pamoja na timu za Aljeria, Morocco na Afrika ya Kati ambapo kati ya timu hizo Algeria na Morocco zilifuzu kucheza fainali hizo, lakini hazikufika mbali.
Wakizungumzia mechi hiyo kwa nyakati toafuti, makocha wa timu hizo, Jan Poulsen (Taifa Stars) na Mutubile Santos wa (DRC), ambaye ni Kocha Msaidizi, walisema wamejiandaa vizuri na watacheza kwa ushindani.
Kwa upande wa Poulsen, alisema kikosi chake kipo katika hali nzuri licha ya kuwakosa wachezaji Juma Jabu, Nizar Khalfan, Ally Badru Ally na Stephano Mwasika na kikubwa watauchukulia mchezo huo kama ni sehemu ya maandalizi yao.
"Katika mazoezi tuliyofanya kwa siku mbili, nimeona wachezaji wangu chipukizi wanacheza kwa kujituma sana, kwani wanashirikiana na wazoefu vizuri,'' alisema Poulsen.
Alisema anatarajia Badru, anatarajiwa kutua nchini leo asubuhi akitokea Misri ila kwa upande wa Nizar, bado hajajua lini atakuja.
Naye Santos aliipaka Stars 'mafuta kwa mgongo wa chupa' kwa kusema kuwa timu hiyo ni nzuri, ambayo kila kukicha inakua kisoka na ndiyo maana wakaichagua kucheza nayo kabla ya kukutana na Shelisheli wiki ijayo.
Alisema na pia kikubwa walichovutiwa kucheza na Taifa Stars ni kutokana na timu hiyo kucheza soka la Kiingereza, mchezo ambao unafanana na Shelisheli.
Kocha huyo alisema katika mechi hiyo hawatakuwa na wachezaji wao wanaocheza soka la kulipwa, ila wengi wanatoka katika timu ya TP Mazembe, DC Motema Pemba, AS Vital na V Club ambapo ana imani wataonesha ushindani mkubwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment