17 February 2012

Simba yapaa Rwanda kufanya mauaji

*Boban, Mwakingwe, Maftah, Kago nje

Na Elizabeth Mayemba

KIKOSI cha Simba kimeondoka nchini jana saa 11 jioni kwenda Kigali, Rwanda kikiwa na msafara wa wachezaji 18, huku wachezaji tisa wakiachwa.

Msafara huo unaundwa na watu 40, pamoja na mashabiki wa timu hiyo ambao wamekwenda kuishangilia.

Simba itashuka uwanjani kesho kucheza na Kiyovu ya Rwanda, katika mchezo wa michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema wachezaji 18 ndiyo walioondoka jana huku tisa wakiachwa kwa matatizo mbalimbali.

Alikitaja kikosi kilichoondoka jana kuwa ni makipa Juma Kaseja na Ally Mustapha 'Bartez', mabeki ni Juma Nyosso, Victor Costa, Obadia Mungusa, Kelvin Yondan, Said Nassoro 'Chollo' na Juma Jabu.

Viungo ni Shomari Kapombe, Patrick Mafisango, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Singano, Jonas Mkude, Salum Machaku na Uhuru Seleman.

Kwa upande wa washambuliaji walioondoka ni Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Christopher Edward na Mkuu wa msafara ni Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu ambaye ameambatana na viongozi wengine.

aliwataja viongozi walioondoka ni Katibu Mkuu Evodius Mtawala, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Ibrahim Masoud na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Francis Waya, pamoja na viongozi wa benchi la ufundi, Kocha Mkuu Milovan Cirkovic na Msaidizi wake Amatre Richard, Meneja Nico Nyagawa, kocha wa makipa James Kisaka na daktari wa timu Cosmas Kapinga.

Kamwaga aliwataja wachezaji walioachwa kuwa ni kipa namba tatu Willbert Mweta, Hassan Hassid, Frank Sekule, Abdallah Seseme, Haruna Moshi 'Boban', Amir Maftah, Ulimboka Mwakingwe, Gervais Kago na Derrick Walluya.

Akizungumzia mchezo wa kesho, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan alisema wana uhakika watafanya vizuri, kwani kambi waliyoiweka Bamba Beach Kigamboni nje kidogo ya Dar es Salaam, waliitumia vizuri.

"Mechi ni ngumu kwani hakuna anayeifahamu Kiyovu, lakini naimani tutashinda mchezo huo wa ugenini," alisema Milovan.




No comments:

Post a Comment