06 February 2012

Namba ya mwisho ni ipi?

MHARIRI naingia, malenga wa uheheni
Naomba nikubalie, majibu yawe hewani
Hakika na mjibi,moyo uwefurahani
Namba ya juu na chini, ndiyo mwisho nakwambia

Master J.C,tulia, kama ndege mtegeoni,
Namba zinaishilia, pale ulipotamani,
Sufuria unaanzia, sio moja niamini.
Namba ya juu na chini,ndiyo mwisho nakwambia

Nina kufunza sikia, mwisho hata themanini,
Utakapo kufikia, hapo ndiyo umewini,
Haina pakuishia, nakuweka darasani
Namba ya juu na chini, ndiyo mwisho nakwambia

Hata kipato sikia,ujue haviwiani,
Hapa ninakugusia, gari na mkokoteni,
Kuna mlaji wa mia, na mwingine milioni.
Namba ya juu na chini, ndiyo mwisho nakwambia

Hesabu ukifikia, hapo mwisho sio deni,
Moja mbili  hadi mia, pia ukipatamani,
Ishia hapo tulia,nakuambia muhoni,
Namba ya juu na chini, ndiyo mwisho nakwambia.

Mbunge niaminia nakuzindua ndotoni
Usidhani nachapia, usikie kwa makini
Swali ninalijibia,kwa uwazi ubaini,
Namba ya juu na chini, ndiyo mwisho nakwambia.

Tamati sijasusia,yakukae akilini,
Tena haitaishia, hata zijae hewani,
Ila mwisho wa dunia, huenda ndio ngamani,
Namba ya juu na chini, ndiyo mwisho nakwambia.

Mubarak.t.Gwanda (Mbunge)
S.L.P 634 Iringa
0762242421/0718833916

*************************
Salamu malenga mikoa mitano

HODI hodi mpangano,Editoria kunipanga
Nitoe yangu maneno, salamu zangu kuchonga
Malenga kwao mkuno, wapate si kuwasonga
Nawasalimu malenga, mikoa hii mitano

Mikoa hii mitano, nawasalimu malenga
Awali LINDI mtuno, siwezi katu kunyonga
Na waje muonekano, malenga tungo kutunga
Nawasalimu malenga, mikoa hii mitano.

KIGOMA kazana mno, uga wa tungo kuringa
Na dagaa mtafuno,mawese kwa kukaanga
Nje tungo si nguno, kutunga mbele kusonga
Nawasalimia malenga mikoa hii mitano

RUVUMA wenye maono, tungo chalia kipenga
Ugani mtafuno,twawahitaji jiunga
Tujenge maelewano, lugha ya wetu wahenga
Nawasalimu malenga,mikoa hii mitano.

KAGERA sio mfano akidhamiri hugonga,
Katoke hasa unono, ni chuo sijakitenga,
Kamishango ni kivuno,kuna malenga watwanga,
Nawasalimu malenga, mikoa hii mitano.

RUKWA nawapa mkono,ndugu zangu Sumbawanga,
Msiwe na mbanano, Onekaneni kulenga,
Na tuwe na upendano, ukuta chama kujenga
Nawasalimu malenga, mikoa hii mitano.

MUHONI ni maagano, beti saba ninapunga
Salamu ya elinino, natoa bila kuvunga
Tufike na mchuano, natoa bila ya kimbunga,
Nawasalimu malenga, mikoa hii mitano.

"Poem Juggler"
Master J.C Muhoni
S.L.P 10960 Mwanza
0786964992
********************
Walemavu na serikali
NCHI yetu ya amani, naitaja Tanzania
Na serikali makini, dunia inatambua,
Iliridhia jamani, mkataba wa dunia,
Serikali iwajali, walemavu Tanzania.

Mahitaji yao mengi,serikali kutambua,
Hoja yao ni wengi, serikali kutambua,
Hoja sio wao wengi, bali haki kutambua
Serikali iwajali, walemavu Tanzania.

Ulemavu tofauti, hapa ninauchambua,
Upo ule wa mafuti, macho masikio pia,
Mikono nayo magoti, viuno ubongo pia
Serikali iwajali, walemavu Tanzania.

Huo wote ulemavu, serikali kuchambua,
Iwe na uvumilivu, katika kusaidia,
Serikali ni sikivu, misada kuwapatia,
Serikali iwajali, walemavu Tanzania.

Iwapate kwa hesabu, na wapi walipo pia,
Watoto kwa mahesabu, ili kuwakadiria,
Ajuza na mashahibu, ni vema kuwatambua.
Serikali iwajali, walemavu Tanzania.

Itembee vijijini, walemavu kuwajua,
Wapitie na mijini, walemavu kutambua,
Shida zao kubaini, ili misada kutoa,
Serikali iwajali, walemavu Tanzania.

Iwapatie elimu, matibabu kazi pia,
Msizitoe hukumu, matatizo kumezea,
Matatizo yasidumu, haraka kuyatatua
Serikali iwajali, walemavu Tanzania

Iwapatie elimu, matibabu kazi pia,
Msizitoe hukumu, matatizo kumezea,
Matatizo yasidumu, haraka kuyatatua,
Serikali iwajali, walemavu Tanzania.

Ujumbe umeshafika, sio kama natania,
Serikali kusifika, haki kiwatolea,
Waovu ikiwashika, sote tutafurahia,
Serikali iwajali,walemavu Tanzania

Mwalimu Vicky Kimaro
Mratibu wa Mradu wa ICD
Wilaya ya Arumeru.
 No comments:

Post a Comment