06 February 2012

NAJUTA SANA

ILIKUWA Siku ya Jumamosi saa nane mchana watu wengi wakiwa wamekusanyika nje ya nyumba ya Mzee Rungu wakisherehekea harusi ya mwanawe Rafael Rungu.
    Nyimbo, ngoma na kila aina ya burudani ilitawalailivyokwa siku ile, mzee Rungu na mkewe, Jamila walifurahi sana kwa kufanikisha vyema sherehe waliyoiandaa.

Ushirikiana, umoja na upendo ndiyo uliofanikisha harusi hiyo kufana zaidi, kwani michango mbalimbali ilichangwa na wanajamii mbalimbali waliokuwa wakiishi katika wilaya ile ya Sumbawanga.

 Kwa kuwa Mzee Rungu alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda miaka ya 80, watu wengi waliweza kumfahamu hivyo michango ya harusi mingine ilitoka Mpanda mkoani Rukwa.

    Rafaeli ama kwa kifupi alitwa Rafa ni mtoto wa tatu kuzaliwa kati ya watoto watano wa Rzee Rungu , alisoma Shule ya Msingi Jangwani iliyopo mjini Sumbawanga hatimaye akaendelea na masomo ya sekondari  katika Shule ya Iyunga mkoani Mbeya. Kwa ujumla masomo yake aliyamudu ilivyo kiasi kwamba hata wazazi wake hasa mama yake alijivuna kwa hilo.

Upendo wa mama yake dhidi yake ulimpa hamasa zaidi ya kupenda masomo, kwa ujumla Rafa alipewa huduma zote za muhimu kutoka kwa mamake japo baba yake pia alimpa huduma lakini ilikuwa kichele,  Rafa hakupendwa sana na baba yake kushinda watoto wengine katika familia ya Mzee Rungu.

Mzee Rungu aliwapenda sana Bakari na Salome, inasemekana Salome alikuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Wasichana Iringa  (Iringa girls) .

Akiwa Kidato cha Pili tu, Salome alianza kuwa mvivu wa kupenda shule na masomo kwa ujumla, akawa mtoro wa kupindukia.

Mara nyingi wanafunzi walipokuwa madarsani wakijisomea, Salome alikuwa akizurura pale mjini akirandaranda huku na huko. Kila siku asubuhi Salome alikuwa akisafiri kwenda Mafinga pindi wenzake wawapo madarasani na jioni kurejea pale shuleni.

Baba yake Salome, Mzee Rungu kila baada ya mwezi mmoja aliweza kumtumia Salome fedha kwa ajili ya matumizi ya kila siku akiwa shule, hivyo fedha aliyokuwa nayo ilimpa kiburi Salome kiasi kwamba hata masomo kuyaona si kitu cha maana kwake.

“Kama ni fedha tunazo za kutosha, sasa nisome ili iweje?” Salome aliwaza siku moja kisha akaendelea kuusemea moyo wake,   “Kilichobaki ni kuponda raha tu, mimi ni mtoto wa mkuu fulani”.

Kwa ujumla Salome alikuwa ni binti wa matanuzi kwani kila week-end hakosi kuhudhuria katika kumbi mbalimbali za starehe hasa disko, kwa kweli usingeweza kuamini kwamba ni mwanafunzi, kwani alijisikia huru kuwa popote wala hakuwa na hofu .

Alijichanganya viwanja mbalimbali kwa kifupi ni kwamba fedha nyingi aliyokuwa akipewa na baba yake alitumia kwa anasa hizo ambazo ni sumu katika masomo.
Mchezo wa kutohudhuria masomo ukawa ndiyo mtindo wake wa kila siku hatimaye mwalimu wake wa darasa aligundua hilo.

Usiku mmoja mwalimu Salimu alipokuwa ndani ya ukumbi wa shimoni pale Mafinga alistushwa na alichokiona mbele yake.

“Jamani nipisheni nipite”, mwalimu Salimu aliwaambia wavulana watatu waliokuwa mbele yake wakicheza muziki akiomba nafasi na kwenda alikokuhitaji.

Ndani ya ukumbi ule wa shimoni kila mtu alikuwa akiburudika kwa muziki uliokuwa ukiporomoshwa na bendi ya TOT PLUS ya jijini Dar es Salaam, hivyo kwa kuwa mwalimu Salimu alikuwa miongoni mwa wakereketwa wa bendi hiyo, aliamua kwenda kujinafasi kwa week-end ile.

Hali kadhalika Salome aliamua kutoroka shule kama ilivyo desturi yake na kwenda Mafinga kuwaona LIVE wana TOT PLUS band.

Bendi ya TOT PLUS ilikonga vilivyo nyoyo za mashabiki wa Mi wa Mafinga na vitongoji vyake kwa ujumla, kwani burudani waliyoipata haikuwa na kifani hivyo kila mmoja aliyekuwepo ndani ya ukumbi alikuwa akicheza wakati bendi hiyo ikitumbuiza.

“Haa! Yule siyo mwanafunzi wangu wa darasa?” Mwalimu Salimu aliwaza na kujiuliza moyo wake na kisha akaendelea kuwaza tena akiusemea moyo wake, “Ni hakika yule ni Salome, amefuata nini hapa ngoja nimfuate”.

Wakati mwalimu Salimu akiwaza yote hayo Salome alikuwa akicheza muziki na mvulana mmoja mrefu na mweupe mwenye nywele ndefu kichwani mwake.
“Wewe acha hizo usione nyapendeza, watu wamegharamia”. Hayo yalikuwa maneno yaliyotamkwa na yule mvulana mrefu aliyekuwa akicheza muziki na Salome, yule mvulana alitamka vile baada ya mwalimu Salimu kumgusa bega Salome.

“Tafadhali kijana, huyu ni mwanafunzi wangu”. Alieleza mwalimu Salimu baada ya kubaini yule kijana amekosa nidhamu kwa kutamka maneno ya kejeli na dharau.
“Salome, shule na starehe bora nini?” Mwalimu alimuuliza Salome.

“Kawaulize wanao”. Alijibu Salome kwa dharau huku akiendelea kucheza muziki.
Ilipotimu saa kumi usiku bendi ilihitimisha burudani na kila mmoja alianza kuondoka katika eneo lile.

Salome aliondoka na yule mvulana mrefu aliyekuwa akicheza naye muziki hali kadhalika na mwalimu Salimu akaondoka zake akielekea maeneo ya pipeline kwa ndugu zake alikofikia.

Ni Jumatatu asubuhi walimu na wanafunzi wapo kwenye uwanja wa matangazo (paredi) Mkuu wa Shule ya Iringa Girls anaonekana kuwa siyo wa kawaida, uso wake umekosa furaha na macho yake yamekuwa mekundu mithili ya pilipili, ama kweli mkuu yule alikuwa amebadilika kwa siku ile.

Baada ya matangazo ya mwalimu wa zamu ndipo alipopewa nafasi ya kuzungumza mkuu wa shule.

“Kuna wanafunzi hapa hawapendi masomo wanaendekeza starehe.”Alieleza mkuu huyo kisha akanyamaza kwa sekunde kadhaa akiyaangaza macho yake huku na huko baadaye akatamka, “Salome pita mbele haraka sana”.

Wakati Salome akisoma Iringa Girls, Bakari naye alikuwa akisoma Shule ya Sekondari Pugu iliyopo jijini Dar es Salaaam akiwa Kidato cha Kwanza. Mwenendo wa masomo haukuwa mzuri kwa upande wake kutokana na ulevi aliokuwa nao.

Bakari alijiingiza katika genge la wahuni pale shuleni, walikuwa wakibwia unga, kuvuta bangi na  kunywa pombe, mbaya zaidi walikunywa pombe haramu wakijihusisha na ubakaji.

Ni kwa kipindi kifupi tu Bakari alijulikana vilivyo pale shuleni kwao japo shule ile ilikuwa na wanafunzi wengi, walikuwa zaidi ya wanafunzi 1500 , ni kutokana na vitendo vyake haramu ndivyo vilivyosababisha ajulikane zaidi kwa kila mwanafunzi.

Utawala wa Iringa Girls uliamua kumfukuza Shule Salome kwa utovu wa nidhamu, Salome hakujua afanye nini, kila alipojaribu kumfuata Mkuu wa Shule akiomba msamaha aligonga mwamba.
Pia alimwendea mwalimu wake wa darasa Bw. Salimu ili amwombee msamaha kwa utawala lakini hakufanikiwa kama siyo kuongezewa maumivu tu.

“Tunakupa muda wa saa nane tu usionekane katika eneo hili la shule, vinginevyo tutakuitia polisi”. Hiyo ilikuwa ni kauli ya mwalimu wa nidhamu akimwamuru Salome aondoke mara moja baada ya kumwona hafanyi kama alivyoelekezwa.

Salome alikwenda bwenini kwake akakusanya kila kilicho chake akaondoka kuelekea stendi kupanda gari. Akiwa ndani ya Coaster Isuzu Journey mawazo tele yalimjia kiasi kwamba hakuelewa wapi aendako.

Gari alilopanda lilikuwa likifanya safari kutoka Iringa mjini kuelekea Njombe mjini. Alipojaribu kuvuta hisia akikumbuka jinsi alivyochezea masomo, machozi yalimlengalenga machoni mwake.

Akiwa bado yupo kwenye dimbwi la mawazo, Salome alistushwa na sauti ya konda aliyekuwa akiomba nauli. “Dada wapi unaenda?” Konda alimuuliza Salome huku akimshika kichwa akimwamsha alipokuwa amejiinamia kwenye kiti.

Salome aliulizwa mara tatu mfululizo lakini hakutoa jibu lolotewapi aendako, hakujua amweleze nini konda, baadaye aliamua kumweleza kuwa anaenda Mafinga.

“Haya nipe buku na mkono”. Konda alimweleza Salome akimaanisha ampe sh. 1500 ikiwa ni nauli kutoka Iringa hadi Mafinga. Kwa kuwa fedha ya ada ya shule hakuipeleka kuilipa hivyo Salome alikuwa na fedha nyingi haikumwia vigumu kutoa nauli.

Akachomoa burunguti la noti akachambua kiasi alichokihitaji akamkabidhi konda.
Saa 9.30 alasiri, Salome aliwasili Mafinga kisha akachukua taksi kuelekea mjimwema kwa yule mvulana aliyekuwa akicheza naye muziki siku ile bendi ilipokuwa ikifanya makamuzi katika ukumbi wa shimoni.

“Dadangu huko mjimwema unakwenda kwa nani?” Dereva taksi alimuuliza huku akiingiza gia vilivyo akiendesha kwa mapozi. “Kwa rafiki yangu”. Salome alijibu.
“Wa kike wa kiume?” Dereva alizidi kuuliza.

“Rafiki ni rafiki tu, awe wa kike au wa kiume haijalishi”. Alieleza Salome akiendelea na zoezi la kuufuta mdomo wake kwa leso.

 “Unajua dada sina lengo baya, nauliza hivyo ili nijue tunaenda kwa nani ili niendeshe moja kwa moja pasipo kubabaika ,” dereva alijibaraguza akachukua kaseti ya muziki na baada ya sekunde chache Celine Dion akasikika kutoka katika kaseti ile.

Dereva taksi alipobaini kuwa dada aliyemchukua si wa masihara kutokana na majibu aliyokuwa nayo, aliamua kunyamaza kimya akicheza tu na usukani wake akiendelea kukanyaga mafuta, gari ile ilipokuwa katika mwendo ndipo Salome alipomwamuru amteremshe akimwonyesha dereva nyumba aendapo.


Itaendelea …


No comments:

Post a Comment