06 February 2012

Kwa nini viongozi wanazidi kujikanganya posho za wabunge?

KILA kukicha suala la posho limekuwa likichukua suala jipya huku kila mmoja akiibuka na kuongea lake.

Viongozi wamekuwa wakitupiana mpira kuhusu suala la posho jambo ambalo limekuwa likiwakanganya wananchi kutokana na viongozi hao ambao wanadhamana kubwa kutokuwa na kauli ya pamoja.

Kutokuwa na kauli ya pamoja kwa suala moja kwa baadhi ya viongozi serikalini kunaonyesha mapungufu na udhaifu mkubwa sana ndani ya serikali.

Japo kila  binadamu ana mapungufu yake lakini ukweli ni kwamba  tunapofanya kazi kwenye taasisi au shirika moja  tunapaswa kuwa makini na mambo kabla ya kuyatoa kwa umma wa Watanzania.

Naweza kusema kutofautiana kwa viongozi hao kunaonyesha wazi kwamba viongozi hao huwa wanafanyakazi pasipo mawasiliano jambo ambalo halipaswi kuwa.

Utakubaliana na mimi kwamba mawasiliano ni kitu cha muhimu sana na ili kazi ziweze kuendelea mawasiliano yanahitajika.

Naamini kwamba kabla maamuzi ya kutangazwa jambo fulani ili umma wa Watanzania wafahamu ni lazima kwanza wahusika wakae na kukubaliana sasa tutasema haya na haya hatusemi.

Nasema kwamba mnawachanganya wananchi katika hili la posho kwa kuwa hivi karibuni  aliibuka Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, na kuwaeleza wahariri wa vyombo vya habari kwamba  jukumu la kuidhinisha ongezeko la posho  ameachiwa yeye na ndiyo mwenye jukumu la kusaini au kutosaini.

Lakini kabla ya Bw. Pinda kusema hayo, alianza Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda kwa kuwaeleza waandishi wa habari kwamba posho zimepanda kutoka sh. 70,000 hadi sh.200,000 na tayari wabunge wamekwishaanza kulipwa.

Bi.Makinda hakuishia hapo aliendelea kuweka wazi kwamba Rais Kikwete ameshatoa kibali chake na mbunge atalipwa katika vikao tu.

Wakati wananchi wa kada mbalimbali wakiendelea kuhoji  na kupinga uhalali huo wa ongezeko la posho za wabunge ,aliibuka tena Bw. Pinda  kwa mara nyingine na  kuwaeleza wabunge kwenye vikao vya utangulizi kwamba tayari Kikwete alikuwa ameidhinisha ongezeko la posho za vikao.

Tukiwa tunaendelea kutafakari hilo, Rais kupitia Kurugenzi yake ya Mawasiliano ilitoa taarifa za kukanusha kwamba  Rais hajabariki ongezeko hilo la posho.

Katika taarifa hiyo iliekeza kwamba  rais anakubaliana na hoja ya nyongeza ya posho kwa wabunge, lakini amewataka wabunge kutumia kikao cha sasa cha bunge kulizungumzia  upya suala hilo.

Kufuatia kutofautiana kwa viongozi hao cha kujiuliza ni nani mkweli kati ya Bi.Makinda, Bw.Pinda na rais na tumuamini nani kwa kile wanachosema.

Naweza kusema ukweli tunaweza kupata kwa wahusika  ambao ni wabunge lakini sina uhakika na hilo kwani hata nao wanaweza kutudanganya kwa kuhofia kwamba wakisema ukweli mwisho wa siku wanawezakuponzwa na ukweli huo.

Suala  la posho sasa limegeuka kuwa  utata mtupu kutokana na viongozi wakubwa kutofautiana kwa kauli na huku kila mmoja akimbebesha mzigo wa lawama mwenzake.

Japo wananchi tunaendelea  kupiga kelele kupinga  nyongeza hiyo lakini hata kama wameanza kupata  potelea mbali lakini  ninachojiuliza hapa ni kwa nini viongozi hao watofautiane, hawaoni kama wanatuchanganya kwa kushindwa kwao kutueleza ukweli.

Binafsi nadhani posho zimeongezwa na wabunge wamekwishaanza kulipwa viwango hivyo, lakini kwa kuwa kila mmoja anaogopa kushutumiwa  ndio maana kauli zao zimekuwa zikitofautiana ili mradi tu watupeleke kisiasa.

Rais ambaye  kwa mujibu wa katiba ndiye muamuzi wa mwisho kwenye suala hilo anaanza kutupa mpira, je, tumueleweje au ndo tusema anakwepa jukumu lake.

Kitendo cha Rais kusema kwamba suala hilo lijadiliwe kwenye kikao cha sasa cha bunge si kuhalalisha, hivi unadhani kweli wabunge  hawa  wa Tanzania tuliowachagua wanaweza wasijiongezee posho hizo?

Inawezekana kweli kumuachia fisi mfupa ili hali unafahamu fika kwamba fisi huyo ana njaa na anautamani sana mfupa huo, sasa suala la rais kuwaachia wabunge kujadili suala la posho, hivi unadhani wabunge hawatapitisha.

Kimsingi sitaki kueleza kama posho ni halali au vipi, ila ni kwa nini viongozi hao wanatofautiana katika kutoa maelezo.

Utata huo unanifanya   niamini kwamba ndani ya serikali kila mtu anaweza kukurupuka kuongea  kile anachoona kinafaa kuongea bila kuwasiliana na wenzake.

Ukweli ni kwamba kinachotakiwa kufanya ili kuepuka kutofautiana ni lazima wahusika wahakikishe kwamba kabla ya kufikia uamuzi wa kuujulisha umma kitu fulani ni lazima mawasiliano yawepo.

Kuwepo kwa mawasiliano baina ya wahusika kutasaidia  sana na hata pale mmoja anapokosea ni rahisi kusahihisha kuliko hili la posho kwani ni vigumu kulisahihisha.

Bw. Pinda, Bi. Makinda na Rais msijikanyage kuhusu suala la posho kama mmeshindwa kutoa maamuzi basi sikilizeni ushauri wa wananchi waliowachagua kwa kuwaunga mkono kuzipunguza zaidi badala ya kuongeza.


No comments:

Post a Comment