20 January 2012

Watoto wanastahili kuendekezwa kielimu

Na Rachel Balama

WATOTO ndio rasilimali yenye thamani kwa vile wao ndio wanaokabidhiwa
maadili na hulka pamoja na maarifa na matarajio ya watu wazima.
Shughuli za watoto, mipango yao na udadisi wao ni mambo yanayofurahisha, kuliwaza na hata kuwajaza hamasa watu wazima hivyo ni haki yao kuandaliwa maisha bora tangu utotoni yatakayowawezesha kucheza vizuri na kujifunza katika hali ya utulifu na amani.
Kwa kutambua umuhimu wa mtoto kwa ustawi wa maendeleo ya taifa ndiyo  maana Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inatekeleza sera ya maendeleo ya mtoto Tanzania ya mwaka 2008.
Sera hiyo ilianzishwa ili kuwafanya wahusika waelewe wajibu na majukumu yao kwa uwazi zaidi na majukumu hayo yatekelezwe ipasavyo ili kuchochea kupatikana kwa haraka ustawi na maendeleo ya watoto wote katika jamii.
Kwa kuwa,  watoto ni sehemu muhimu ya jamii na ndiyo tegemeo la uendelevu wa taifa lolote, kwa sababu hiyo watoto hawana budi kulelewa vizuri na kuendelezwa.
Watoto wanayo mahitaji ya msingi ambayo yanahalalisha kuwepo kwa mipango maalum inayowalenga wao tu.
Mipango hiyo hujumuisha chanjo ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, elimu ya awali, elimu ya msingi na elimu ya sekondari.
Ingawa lishe bora ni muhimu kwa kila binadamu lakini ni muhimu zaidi kwa watoto ili kuwawezesha kukua ipasavyo kimwili na kiakili.
Mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yaliyotokea mara baada ya sera ya Maendeleo ya mtoto kuanza kutekelezwa mwaka 1996 yamesababisha sera hiyo kufanyiwa marekebisho ili kuendana na hali halisi ya mazingira yaliyopo.
Mabadiliko mengi kama ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya UKIMWI na athari zake, utandawazi, mfumo wa biashara huria na mmomonyoko wa maadili ya jamii ni mingoni mwa mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa  ili kulinda ustawi wa mtoto huyo.
Mabadiliko hayo  yanatoa changamoto mpya katika kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa watoto wote.
Ukweli ni kwamba, malengo ya Milenia ya mwaka 2000 yalizingatia kuwa ifikapo mwaka 2015 watoto wote kupatiwa elimu ya msingi na kupunguza vifo vya watoto.
Japo bado muda upo lakini cha kujiuliza kwamba bado Kwa hili serikali imepiga hatua lakini japo bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili watoto  ambazo kama hazijatatuliwa zinaweza kusababisha watoto kutokuwa na misingi mizuri kwa baadaye kwa kuwa wao ndio taifa lijalo.
Ni wazi kabisa kuna sera nzuri za watoto lakini bado utekelezaji wa sera hizo unasuasua kutokana na sababu mbalimbali.
Kimsingi kukua kwa mtoto kiakili ni kuongeza upeo, uelewa, ufahamu, ubunifu na udadisi juu ya mambo mbalimbali katika mazingira yake kadri umri unavyoongezeka.
Katika kumuendeleza huko kiakili mtoto viashiria vya uandikishaji wa watoto katika elimu ya msingi vinaonesha kuwa, kwa miaka mingi iliyopita lilikuwa asilimia 50 kiwango ambacho ni kidogo ukilinanisha na mwaka 2002 ambapo walikuwa asilimia 80.7.
Japo kwa sasa kiwango hicho kimepanda lakini cha kujiuliza je watoto hao ambao uandikishwa kuanza darasa la kwanza wanapatiwa elimu bora.
Kutokana na mazingira ya shule, tumeshuhudia watoto wengi wanaomaliza elimu ya msingi baadhi yao hawawezi kusoma na hata kuandika.
Na wale wanaojua kusoma na kuandika  ni kutokana na juhudi za wazazi wao kwa kuwatafutia sehemu za ziada kwa ajili ya kujisomea.
Ukweli watoto wanapaswa kuandaliwa mazingira mazuri katika kila nyanja kwa lengo la kuimarisha ustawi wa maendeleo ya jamii.
Mbali na watoto kupata haki ya kuwezeshwa kiakili, watoto pia wanahitaji ulinzi dhidi ya kazi nzito zisizowiana na umri wao.
Pia kudhulumiwa mali zao hasa kwa watoto yatima, kutupwa au kutelekezwa na wazazi, kuonewa, kupuuzwa na kukoseshwa au kupoteza uraia ni sababu ambazo zinachangia watoto hao kukosa raha .
Ili kumuandaa mtoto katika mazingira mazuri, anahitaji ulinzi dhidi ya unyanyasaji, vitendo vya ukatili kama vile ukeketaji watoto wakike au kuwalazimisha kuoa au kuolewa katika umei mdogo.
Watoto wanatakiwa kukingwa na matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya ubakaji, kwani utafiti uliofanywa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora mwaka 2005 unaonyesha kuwa  vitendo vya kutekeleza watoto vinaongoza kwa asilimia 32, unyanyasaji wa kijinsia asilimia 29, ukatili wa kudhuru wmili alimia 26 na asilimi 29 vitendo vya maudhi na unyanyasaji.
Ili watoto hao waweze kukua katika mazingira mazuri, jamii, wadau mbalimbali, walezi pamoja na wazizi hawana budi kuhakikisha kuwa vitendo hivyo havitokei.
Japo Tanzania kwa kushirikiana  na Shirika la Kazi Duniani(ILO) zimekuwa zikiendasha kampeni ya kuelimisha jamii kupiga vita ajira za watoto lakini bila ushirikiano toka kwa jamii vitendo hivyo vitaendelea kutokea.
Licha ya  ushiriki wa watoto katika maendeleo kutiliwa mkazo katika mikataba, kanuni na sheria mbalimbali bado watoto hawapati haki kama zinavyostahili.

No comments:

Post a Comment