23 January 2012

Sumari kuagwa leo Dar

Na Waandishi Wetu

MWILI wa Mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM) Bw. Jeremiah Sumari, unatarajiwa kuagwa leo
katika Kanisa la Kiinjili la Kirutheli (KKKT) Msasani, Dar es Salaam na baadaye kupelekwa katika Ukumbi wa Karimjee kwa heshima za mwisho.
Viongozi wa serikali, dini na vyama vya siasa nchini wanatarajiwa kuhudhulia ibada ya misa takatifu kanisani hapo na baada ya kuagwa kwa mwili huo utasafirishwa Jumapili asubuhi kwenda kijijini kwao Akeri, Meru mkoani Arusha kwa mazishi yatakayofanyika Jumatatu.
Akizungumza na Majira nyumbani kwa marehemu Mbezi, Dar es Salaam  jana, msemaji wa familia hiyo Bw. Emmanuel Olekambainei alisema kuwa, taratibu zote za kuaga mwili wa marehemu zimekamilika.
Alisema, kabla ya mauti yake, mbunge huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani ya ubongo ambapo aliwahi kutibiwa nchini India zaidi ya mara mbili.
Aliongeza kuwa, mwaka 2010 alikwenda India na kupatiwa matibabu na baadaye alirejea jimboni kwake na kufanya kampeni kabla ya hali yake kubadilika.
Bw. Olekambainei alisema kuwa, baada ya kubadilika kwa hali yake, mbunge huyo alikwenda nchini Kenya kwa ajili ya kupima afya yake kabla ya kurejea tena India na kisha kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) kwa uchunguzi zaidi hadi mahuti yalipomfika.
Makada wa CCM kutoka Tawi la Malecela lililopo kando ya nyumba ya Marehemu Sumari walisema kuwa, wameguswa na msiba huo wa mwanachama mwenzao kutoka na mchango wake wa hali na mali.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama hao, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Tawi la Malecela Bw. Juma Mponda alisema kuwa, wamepokea msiba huo kwa simanzi kubwa huku akiacha pengo lisiloweza kuzibika.
Viongozi waliohudhuria msiba huo ni pamoja na Waziri wa Fedha Bw. Mustafa Mkulo, Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah na makada mbalimbali wa chama hicho.
Marehemu Sumari alifariki juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na saratani ya ubongo, mbunge huyo ameacha mjane, watoto wanne, na wajukuu saba.

No comments:

Post a Comment