23 January 2012

Uzembe wa viongozi wadaiwa kuwanyima haki wananchi

Na Zuhura Semkucha, Shinyanga

VYAMA vya siasa hapa nchini vimetupiwa lawama kwa kuwakumbatia viongozi wenye

matatizo ambao wanashindwa kuwajibika kwa wananchi kwa sababu ya maslahi yao binafsi.
Madai ambayo yalidaiwa kuwa viongozi wengi huwa hawawajibiki kwa sababu wameingia kwenye madaraka kwa njia tofauti ikiwemo ya rushwa.
Madai hayo yalitolewa na Diwani wa Kata ya Mwadui Luhombo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Bw.Paulo Magembe wakati akichangia mada kwenye mkutano kuimarisha mahusiano kati ya viongozi waliochaguliwa na kuteuliwa na jamii sambamba na uwajibikaji kwa ufadhili wa Shirika la The Foundation for Civil Society chini ya uratibu wa Mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali mkoani humo (SHINGONET).
Alisema, kutokuwajibika kwa viongozi kwa kiasi kikubwa kunatokana na jinsi walivyochaguliwa kwa sababu utaratibu wa kuwachagua hadi watoe zawadi kwa wananchi hivyo hakuna kinachofanyika zaidi ya kujinufaisha wao.
"Huwezi kumuuliza swali kiongozi aliyechaguliwa, kwa sababu wakati wa mchakato wa kumpata alitupatia zawadi kidogo, sasa kwa mtindo huu daima hatutakuwa na viongozi wawajibikaji bali wananchi kila siku tutakuwa tunalalamika tu," alisema.
Bw.Magembe alisema, wananchi wanatakiwa kujua kuwa viongozi waliowachagua
wanapaswa kuwajibika kwao na si wao ndio wawajibike kama ambavyo wanafanya kwa sasa, kwa kumtetemekea kiongozi waliyempigia kura kwa kushindwa kumuhoji anawajibika tuliyempigia kura kwa kushindwa kumuuliza anawajibikaje kwetu.
Alisema, wananchi wengi hawafahamu uwajibikaji wa viongozi ndio maana
wanaendeshwa na viongozi kadri wanavyotaka wao kwa sababu ya madaraka yao ambayo wamepewa jambo ambalo si sahihi hivyo wananchi watambue kuwa wao ndiyo wenye jukumu la kuwaendesha viongozi na si vinginevyo.
Pia alisema, Serikali itunge sheria kuwa mbunge anaposhindwa kufanya kazi
wachukuliwe hatua kwa sababu kwa upande wa mwenyekiti wa kijiji, kata wanapokosea kidogo tu wanawajibishwa hivyo sheria itungwe kwa wabunge.

No comments:

Post a Comment