23 January 2012

Viti maalumu CCM watakiwa kuiga wenzao wa CHADEMA

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

WABUNGE wa viti Maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuiga mfano
wa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao wamekuwa wakichangia kiasi cha sh.100,000 kila mwezi kwa ajili ya kusaidia jumuiya za wanawake ndani ya chama chao.
Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT), Bi.Sofia Simba wakati akifungua mkutano wa mafunzo ya siku mbili kwa makatibu wa wilaya na mikoa wa jumuiya hiyo ya umoja wa wanawake nchini shughuli ambayo ilifanyikia mkoani Dodoma.
Bi.Simba alisema, jumuiya hiyo ya umoja wa wanawake lazima isaidiwe na wabunge wa viti maalumu wanawake kwa kuwasaidia kutoa kiasi cha sh.100,000 kwa kila mwezi lakini akabainisha kuwa jambo hilo limekuwa halifanyiki kutokana na wabunge wengi wa viti maalumu kutotekeleza jambo hilo.
“Hapa nataka niseme kuwa wenzetu wabunge wa viti maalumu hasa wa Chadema wamekuwa wakifanya vizuri katika utekelezaji wa jambo hili, kwani kila mwezi wamekuwa wakitoa fedha hizo kwa ajili ya kuzisaidia jumuiya zao kwanini, na sisi wabunge wa viti maalumu wasitekeleze hilo kwa kuwasaidia, hivyo mnachotakiwa ni kuwa waadilifu katika masuala ya fedha na kuwafuatilia kwa karibu,” alisema
Alisema, wabunge wa viti maalumu wapo wengi hivyo wangechangia kiasi hicho
katika jumuiya hiyo ya wanawake wangeweza kupata fedha nyingi kwa kuwa wale wa Chadema wameweza kufikia hapo walipo kwa kuwa huwa wanajitolea.
Hata hivyo, Bi.Simba alisema, amekuwa akipata taarifa kuwa ni kwanini wabunge hao wa viti maalumu hawachangii fedha zao katika jumuiya hiyo na kusema kuwa wengi wao wanadai kuwa hawafuatwi ili kudaiwa fedha hizo lakini wengine wanadai kuwa fedha hizo zikichangiwa katika jumuiya hiyo zinaliwa.
Kutokana na changamoto hizo pia mwenyekiti huyo alilazimika kuwaeleza wajumbe hao ambao ni makatibu wa wilaya na mikoa wa jumuiya hiyo ya wanawake Tanzania
kuhakikisha kuwa wanafuata kanuni za fedha  kwa kutoa risti pindi mtu anapotoa fedha pamoja na kuzisimamia fedha hizo vizuri.
Akizungumzia suala la kuingiza wanachama katika jumuiya hiyo alisema, kuwa wakati umefika kwa jumuiya hiyo kuingiza wanachama wengi na hasa wasomi na wale wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali ili kuifanya jumuiya hiyo kwenda na wakati.
Alibainisha kuwa wakati huu si wa kufanya kazi kwa mazoea kwani ni wakati wa
mabadiliko hivyo wanawake lazima wabadilike na kujieleimisha zaidi ili waweze
kupata nafasi za uongozi ndani ya jumuiya hiyo na hata katika chama.
Bi.Simba akizungumzia suala la umoja aliwataka wanawake hao kujenga mshikamano na kuwaonya wanawake hao kutojiingiza katika masuala ya uanaharakati kwa kukikosoa chama na serikali badala ya kujibu mapigo yanayotolewa na wapinzani.
Alisema, yapo mambo mengi ambayo wapinzani wamekuwa yakiyazungumza na chama chao kimekuwa kikisemwa vibaya lakini wanawake hao wamekuwa kimpya jambo ambalo alisema, wanapaswa kutafuta taarifa za kujibu mapigo na wasikalie kulalamika tu.

No comments:

Post a Comment