24 January 2012

TFF yaomba makato U/Taifa yapungue

*Twiga Stars kukipiga Wabunge

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeiandikia barua serikali kuomba ipunguze gharama za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya marudiano kati ya timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars) na Namibia, itakayochezwa Januari 29, mwaka huu.

Mbali na hilo, timu hiyo inatarajia kushuka uwanjani Alhamisi kuumana na  Wabunge wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, katika mechi ya hisani itakayochezwa kwenye Karume, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo Boniface Wambura, alisema wameiandikia barua serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo waondoe gharama za uwanja kama moja ya msaada wao katika mechi hiyo.

"Unajua kuutumia uwanja ule ni gharama sana, sasa sisi tunaomba watuondolee gharama za usafi, ulinzi ambazo zinakaribia sh. milioni 1, zile za kuwalipa wachina ambazo karibu sh. milioni 2, kuna asilimia 10 ya uwanja na maandalizi ya uwanja," alisema Wambura.

Pia Wambura aliongeza kwamba, timu hiyo Alhamisi itacheza na wabunge katika mchezo maalumu wa hisani kwa ajili ya kutafuta fedha, zitakazoisaidia timu hiyo kujiandaa na mechi yao dhidi ya Namibia.

"Hilo kama shirikisho tumelikubali na mechi hiyo itapigwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na baada ya mchezo huo wabunge watatoa walichonacho na hiyo itakuwa ni moja ya msaada kwa timu na pia kucheza nayo itawasaidia wachezaji wa Twiga, kujiweka sawa," alisema.

Alisema bado wanasisitiza kampuni na taasisi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuisaidia timu hiyo, katika maandalizi yake licha ya kwamba baadhi ya wadau wa soka wameshaanza kujitokeza, lakini misaada bado haitoshi.

Twiga Stars katika mechi ya marudiano inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote, ili kusonga mbele hatua inayofuata ambapo itakutana kati na Misri au Ethiopia.

Mechi ya kwanza iliyopigwa Winghoek, Namibia Twiga ilichomoza na ushindi wa mabao 2-0, mabayo yaliyofungwa na Mwanahamisi Omari na Asha Rashid.

No comments:

Post a Comment