19 January 2012

Nchambi amshtaki Waziri Ngeleja Ofisi Kuu CCM

Na Rachel Balama

MBUNGE wa Kishapu, mkoani Shinyanga, Bw. Suleiman Nchambi, amemshtaki Waziri wa Nishati na Madini,
Bw. William Ngeleja, kwa uongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bw. Ngeleja anadaiwa kuwakimbia wapiga kura katika mkutano uliokuwa ufanyike kwenye Kata ya Songwa, kujibu hoja za wakazi zaidi ya 30,581 wanaodai kutonufaika na mgodi wa almasi wa Mwadui.
Habari za uhakika kutoka ndani ya chama hicho, zinasema tayari Bw. Nchambi, amefikisha malalamiko hayo kwa Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Wilson Mukama ambapo Sekretarieti ya Taifa ya chama hicho ilikuwa ikutane jana kujadili suala hilo.
Chanzo chetu cha habari kimesema kuwa, kitendo cha Bw. Ngeleja kutohudhuria kikao hicho, kinachangia kudhoofisha nguvu ya chama jimboni humo na kusababisha wapiga kura kumchukia mbunge wao ndio maana Bw. Nchambi, ameamua kulifikisha suala hilo katika ngazi ya juu.
Majira lililopuuliza Bw. Nchambi kama kweli amepeleka malalamiko kwa Bw. Mukama alikiri kufanya hivyo kwa madai kuwa, hajaridhishwa na hatua ya Bw. Ngeleja kuwakimbia wapiga kura jimboni humo na kujibu maswali yao.
Aliongeza kuwa, Novemba 2011, alimuomba Bw. Ngeleja kufika katika kata hiyo ili azungumze na wachimbaji wadogo wadogo ambao walijiandaa kuonana nae ili wamweleze kero zao.
Januari 15 mwaka huu, Bw. Ngeleja alikuja Kishapu na mimi nilimuomba aende Songwa kuonana na wananchi, yeye alikubali kufanya hivyo na mimi nilifikisha taarifa kwa wahusika.
Niliwaeleza wananchi na viongozi wa kata juu ya ujuio wa Bw. Ngeleja, siku moja kabla nilipokea taarifa kutoka kwa msaidizi wa Waziri akidai ratiba imebadilika,¡± alisema.
Bw. Nchambi aliongeza kuwa, taarifa hiyo ilisema Bw. Ngeleja hata onana na wananchi wa Kata ya Songwa badala yake ataenda Kata ya Mondo, Kijiji cha Buganika.
Nilimpigia simu mara kadhaa akawa hapokei kitendo ambacho sikukifurahia, wananchi walikiamini chama chetu ndio maana wanakichagua lakini kitendo cha Bw. Ngeleja kuwakimbia wananchi kinabomoa chama,¡± alisema Bw. Nchambi.
Aliongeza kuwa, ziara aliyofanya Bw. Ngeleja kwenye Kata ya Mondo, ilipangwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Bw. Abdallah Lutavi.
Alisema katika mazingira ya aina hiyo, yupo tayari kujiuzulu ubunge na kurudisha kadi ya CCM kwani Bw. Ngeleja na Bw. Lutavi wanakichimbia chama hicho kaburi.
Bw. Ngeleja alipoulizwa kuhusu madai hayo alikiri kufanya ziara ya kiserikali wilayani humo na kudai kuwa, ratiba ya ziara hiyo hajaipanga yeye bali imepangwa na uongozi wa Wilaya.
Kawaida mawaziri wanapokuwa kwenye ziara, huwa wanapangiwa ratiba na wenyeji, hivyo ukitaka kujua zaidi wasiliana na uongozi wa Wilaya kwani mimi nilikuwa nafuata ratiba,¡± alisema na kuongeza kuwa, pengine wananchi hao wana shauku ya kumuona.
Kwa upande wake, Bw. Lutavi alipoulizwa kuhusu sakata hilo, alisema Wilaya yake ina miezi mitatu hakuna mkutano uliofanyika  au ziara iliyomuhusu Waziri.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, alipoulizwa kama suala hilo limefikishwa kwa Katibu  Mkuu, alisema hana taarifa zozote.
Naomba unipe nusu saaa nilifuatilie nitakupa majibu,¡± alisema Bw. Nnauye lakini alipopigiwa simu kwa mara ya pili, ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

No comments:

Post a Comment