19 January 2012

Mgomo wa malori

Waajiri wanaoghushi mikataba kufikishwa mahakamani

Na Mwandishi Wetu, Tunduma

WAMILIKI wa magari makubwa ya mizigo yaendayo nje ya nchi
ambao watabainika kughushi mikataba ya madereva wao, watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Adivocate Nyombi aliyasema hayo jana mjini Tunduma wakati akizungumza na madereva hao na kuwaomba wasitishe mgomo.
Wapo baadhi ya wamiliki wa magari ambao wamekuwa wakienda katika Ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), kupeleka mikataba yenye majina ya bandia, kama tukiwabaini tutawakamata na kuwafikisha mahakamani,¡± alisema Kamanda Nyombi.
Aliongeza kuwa, mwajiri mwingine anaweza kwenda na mkataba unaoonesha jina la mtu mwingine wakati tayari amemfukuza kazi au amerafiki dunia jambo ambalo kisheria ni kosa.
Alisema mwajiri ambaye atabainika kufanya hivyo, atafikishwa mahakamani kwa makosa ya kugushi na kuidanganya serikali.
Kamanda Nyombi aliwaomba madereva hao wasitishe mgomo kwani watasababisha kuvunjika kwa amani katika eneo la mpakani na kukwamisha shughuli za kijamii.
Serikali inashughulikia madai yenu kwani hadi Desemba 2011, SUMATRA imetoa leseni baada ya kusaini mikataba 2,655, asilimia kubwa ya madereva wana mikataba na wachache hawana,¡± alisema.
Aliwataka madereva hao kujaza fomu zilizotolewa mamlaka hiyo ili kusaidia kuwabaini waajiri wadanyanyifu kupitia mikataba hiyo.
Nawaomba mjaze fomu hizo kama wenzetu SUMATRA walivyo tuambia, ndani ya mwezi mmoja mtakuwa umepata mikataba yenu,¡± alisisitiza Kamanda Nyombi.
Wakati huo huo, Serikali mkoani hapa chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Mkoa Bw. Abbas Kandoro, jana waliendelea na kikao cha kutafuta muafaka na viongozi wa viongozi wa madereva hao ili kumaliza mgomo ambao umedumu kwa siku tatu hadi sasa.
Taarifa zilizotufikia wakati tukienda mtamboni zinasema kuwa, madereva hao wamekubali kusitisha mgomo kutokana na ahadi ya Serikali kushughulikia madai yao ndani ya mwezi mmoja.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu kutoka Tunduma, Mwenyekiti wa madereva hao, Bw. Rashid Salehe, alisema lengo lao ni kutaka kuhakikisha madereva wote wanakuwa na mikataba bora inayoweza kuboresha maisha yao.

No comments:

Post a Comment