13 January 2012

Naipongeza serikali kuruhuru wanafunzi kurudia mitihani

Na Rachel Balama

DESEMBA 14, mwaka jana serikali ilitangaza matokeo ya darasa la saba ambayo kati ya wanafunzi 983,545 waliofanya mtihani huo, 567,767 sawa na asilimia 58.28 walifaulu huku  ikifuta matokeo ya watahiniwa 9,736.

Miongozi mwa waliofutiwa matokeo hayo, wanafunzi 94 walikamatwa na karatasi za majibu, wanne walibainika kuandikiwa majibu, tisa walibainika kukariri darasa kinyume na utaratibu na 9,629 walibainika kuwa na majibu yenye mfanano usio wa kawaida.

Hata hivyo mara baada ya watahiniwa hao kufutiwa mitihani hiyo, wazazi, walezi na wadau walilalamikia hatua hiyo kwa kile walichodai kuwa ni ukiukwaji wa haki za msingi za wanafunzi kupata elimu.

Kitendo cha watahiniwa hao kufutiwa matokeo binafsi si cha busara kwa kuwa tunatambua kwamba elimu ndio suruhu ya matatizo na ndiyo msingi wa maisha bora kwa binadamu.

Tunafahamu kabisa binadamu yoyote bila kuwa na elimu maisha yake hapa duniani yatakuwa ya kubangaiza kwa kuwa elimu inamuwezesha mtu kutoka sehemu moja na kufikia sehemu nyingine ambayo ni bora.

Hata hivyo baada ya wadau mbalimbali kupiga kelele, serikali iliamua kwamba watahiniwa 9,629 waliofutiwa matokeo ya mtihani huo uliofanyika mwaka jana baada ya kugundulika kufanya udanganyifu, warudie mtihani huo Septemba mwaka huu.

Serikali ilisema uamuzi huo unawahusu  wanafunzi wale tu waliogundulika kuwa na majibu yenye mfanano usio wa kawaida na kwamba aumuzi huo hautawagusa wanafunzi 107 ambao walifutiwa matokeo yao baada ya kukutwa na majibu.

Hatua ya  serikali imekuja baada ya kuona kiwango kikubwa cha watahiniwa kufutiwa matokeo hali inayoweza kupelekea wanafunzi hao kujiingiza katika makundi mabaya pale wanapokuwa nyumbani hali ambayo inaweza kuwasababisha wanafunzi hao utegemezi wanapofikia utu uzima .

Mbaya zaidi kifungu  cha sheria namba  52(b) kinasema kwamba mwanafunzi wa darasa la saba akifutiwa matokeo hatakiwi kuendelea  na masomo na hiyo inakuwa ndio  lala salama.

Japo wanafunzi hao watarudia mitihani hiyo sanjari na wenzao mwezi Desemba mwaka huu, lakini binafsi naipongeza hatua hiyo ya serikali kwa kutambua umuhimu wa elimu na kuona kwamba watoto hao wangeishia kuzuriura mitaani na hivyo kutengeneza majjambazi na machangudoa wa baadaye.

Kwa kuwa watahiniwa ni wengi serikali imefanya aumuzi mzuri wa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata elimu.

Serikali imefanya jambo la maana na la muhimu sana kwa kuwaruhusu wale ambao majibu yao yalikuwa na mfanano usio wa kawaida kurudia masomo na wenzao Septemba mwaka huu.

Hata hivyo mbali na watahiniwa hao kuruhusiwa kurudia mitihani lakini angalizo kwa serikali inapaswa kuwa makini katika kusimamia uchakachuaji wa mitihani.

Vitendo vya ukakachuaji wa mitihani vinashamiri sana na hiyo inatokana na watendaji husika kutokuwa waaminifu katika kazi zao.

Hata hivyop naamini kabisa wanaofanya uchakachuaji huo si wanafunzi bali ni mtandao wa watu fulani kuanzia wachapishaji, walimu, walinzi na n.k.

Ili kukomesha vitendo vya udanganyifu katika mitihani ni lazima wadau wote kushirikiana pale mnaposikia taarifa za kuvuja kwa mitihani kabla haujafanywa.

Mara nyingi mitihani inapochakachuliwa hata kama watu wanajua kinachoendelea wamekuwa wakikaa kimya lakini  inapotolewa adhabu kwa wanafunzi watu hao ulalamika.

Ukweli kabisa kulalamika pekee hakusadii kitu kinachotakiwa kwa pamoja jamii tushirikiane na serikali  kufichua maovu kabla hayajaleta athari kwa jamii.

Watanzania tunapaswa kuunga mkono jitihada hizo za serikali za kutaka wanafunzi hao kurudia mtihani kwa kuwa ni vizuri kurudia kuliko kukaa majumbani pasipo kuwa na muelekeo.

Hata hivyo mbali na serikali kutawa wanafunzi hao kurudia mitihani, walimu, wazazi na wadau wengine tunapaswa kujifunza katika hilo.

Kwa kuwa nina imani kabisa nyie ndio chanzo kikubwa cha kusababisha wizi wa mitihani na mwisho wa siku mnakuwa mnalalamika.

Wazazi kwa upande wao wanachangia udanganyifu katika mitihani kwa kushirikishwa na walimu wasio waaminifu ili matokeo yanapotoka shule iweze kusifiwa kwamba imefaulisha wanafunzi wengi kumbe ni kujidanganya.

Shule ikisifiwa imefaulisha wanafunzi wengi kwa kufanya udanganyifu katika mitihani huo ni ujinga na hatimaye mwisho wa siku inapogundulika athari zinawakuta wanafunzi na si walimu.

Serikali pia inatakiwa kujifunza katika  hilo na  kufanya kazi katika utaratibu unaoeleweka la sivyo kila mwaka tutasikia udanganyifu wa mitihani ukifanyika.

Kwa upande wa wanafunzi msikubali kila mnachotakiwa kufanya na walimu kwa kuwa mwisho wa siku nyie ndio mnaopata machungu kwa kufutiwa mitihani.

Sioni sababu ya nyie kukubali kupewa majibu ili mradi tu mfaulu, tumieni akili zenu kuliko kufanya udanganyifu.

Kwani hata kama serikali ingewaacha muendelee na elimu ya sekondari kama kweli mlipewa majibu huko mbeleni ni lazima mngeshindwa tu.

No comments:

Post a Comment