24 January 2012

Madini ya shabaghafi, jasi yagundulika Singida

Na Thomas Kiani
Singida

WIZARA ya Nishati na Madini kupitia ofisi ya madini Kanda ya Kati Singida imeanza  mchakato wa kutoa elimu  kwa wananchi wa Mkoa wa Singida kuhusu rasilimali za madini ziliyoko kwenye mkoa huo baada ya kugundua kuwepo kwa madini ya shaba na Jasi wilayani Iramba na Manyoni.


Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari liyopita Kamishina Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati Singida Bw. Manase Mbasha alieleza  Mkoa wa Singida una rasilimali
nyingi za madini yenye tija kwa maendeleo ya mkoa na taifa lakini unakabiliwa na changamoto nyingi katika sekta ya madini zikiwepo utafiti, utaalamu, uchimbaji
vitendea kazi vya kisasa, miundo mbinu, mikopo na soko zuri la madini.

Kamishina Mbasha alisema Mkoa wa Singida una madini mengi katika baadhi ya maeneo yake lakini madini ya dhahabu ndio yanayopatikana katika maeneo mengi hata kabla ya vita vikuu vya dunia kulikuwa na migodi ya dhahabu wilayani Iramba iliokuwa ikimilikiwa na serikali ya Uingiereza na iliendesha utafiti wa madini hayo na mengine hadi mwaka 1962.

Katika taarifa yake Kamishina Mbasha alithibitisha kugunduliwa kwa madini ya shaba
ghafi kata ya Ibaga Tarafa ya Kirumi Wilayani Iramba na baada ya utaratibu, utafiti
na utaalamu kukamilika uchimbaji wake utaanza mara moja kwa sababu madini ya shaba
 soko lake liko wazi.

Mbasha aliendelea kusema kuwa madini ya jasi yamegundulika wilayani Manyoni Kata ya
Itigi na tayari serikali iko katika hatua za mwisho katika mikakati ya uchimbaji na
kutafuta soko la uhakika kwenye viwanda vya simenti vya ndani na nje ya nchi.

Mhandisi wa migodi Kanda ya kati Singida Bwana Gabriely Senge katika taarifa hiyo
amesema mabadiliko mbali mbali ya Kisera na utawala, serikali iliamua kweka
kipaumbele katika utafiti na uchimbaji wa madini kote nchini na kufungua ofisi za
madini karibu kila mkoa ili kutoa leseni ndogo na kubwa na kutoa vibali kwa
wachimbaji wadogo, watu binafsi na Makampuni.

“Mchakato mkubwa wa serikali hivi sasa ni kuweka mikakati ya nguvu kuhakikisha kila mwananchi popote pale alipo anaondokana na umaskini kwa njia zote halali za kiuchumi kwa kutumia rasilimali za madini, misitu, ardhi na bahari,” alisema Senge.

Mhandisi Senge alidokeza kwamba bado kuna maeneo mengi mkoani Singida ambayo hayajafanyiwa utafiti wa kina na imeamua kulifufua Shirika la utafiti na uchimbaji
madini taifa “STAMICO” ili liweze kuwasaidia wachimbaji wadogo utafiti, utaalamu,
mikopo na kuwapa wachimbaji hao vifaa vya kisasa vya uchimbaji ili madini wanayopata
yapate bei nzuri kwa kuthamanishwa.

No comments:

Post a Comment