25 January 2012

CAF yairudishia TFF mzigo wa Simba, Yanga

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limesema halina matatizo na mechi za marudiano za kimataifa za Simba na Yanga, kusogea mbele ila Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), lizungumze na vyama vya soka vya nchi husika.

Hatua hiyo ya CAF, imekuja baada ya TFF kuiandikia barua kuomba mechi hizo zisogee mbele kutokana na Februari 29, timu ya Taifa (Taifa Stars) itaumana na Msumbiji katika mechi za mchujo wa kuwania kufuzu Mataifa ya Afrika kwa 2014.

Simba na Yanga zilipangwa kucheza mechi zao za marudiano dhidi ya Kiyovu ya Rwanda na Zamaleki ya Misri kati ya Machi 2,3 na 4 mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo Boniface Wambura, alisema juzi wamepokea taarifa kutoka CAF ikielekeza kwamba wao hawana tatizo na mechi hizo, kusogea mbele ila wanapaswa wazungumze na wahusika kuona kama inawezekana.

“Tunashukuru CAF wamekubali katika hilo, ila tunapaswa kuzungumza na FA ya Misi na Rwanda juu ya jambo hilo na tayari tumeshawatumia barua ya maombi, hivyo tunasubiri majibu yao kuona itakuwaje,” alisema Wambura.

Alisema sababu kubwa ya kuomba mechi hizo zisogee mbele ni kutoa nafasi kwa wachezaji wa timu hizo, kupata muda wa kupumzika ili pia wapate muda mzuri wa kuzitumikia timu zao kama mechi hizo zitasogea mbele.

Wambura alisema mechi ya Taifa Stars itapigwa Februari 29 alafu Machi 2, 3 au 4 wachezaji hao hao wanatakiwa kwenda kucheza mashindano mengine makubwa kitu ambacho si kizuri, hivyo kama zitasogezwa mbele itakuwa vizuri zaidi.

Katika hatua nyingine, Wambura alisema Kamati ya Mashindano iliyokutana juzi kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Ligi Kuu Bara, imeamua kubadili baadhi ya michezo ya ligi hiyo.

Aliitaja baadhi ya michezo hiyo ni uliokuwa wa Toto African ya Mwanza dhidi ya African Lyon uliotakiwa kufanyika Februari 5, mwaka huu sasa utapigwa Aprili 18 na ule wa Aprili 18 kati ya Villa Squad na Lyon sasa utapigwa Aprili 22, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment