*Wanachama viongozi kung'atuka
Na Mwali Ibrahim
BAADHI ya wanachama wa Yanga, wameutaka uongozi wa klabu hiyo kujiuzulu, kutokana na kushindwa kuiongoza. Hali imekuja kutokana na kauli ya Kocha Mkuu wa
klabu hiyo, Kostadin Papic mwanzoni mwa wiki kukaririwa na vyombo vya habari akilalamika kwamba wamekumbwa na ukata huku viongozi wakiwa wamemtenga.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Msaidizi wa tawi la Umoja la Tandale, Said Bakari mwenye kadi namba 003544 alisema viongozi hao wanaiendesha Yanga, bila mpangilio na kwa zaidi ya mwaka haina mfadhili zaidi ya kuitegemea Kampuni Bia Tanzania (TBL).
Alisema imefikia hatua hata fedha za kuweka mafuta gari kwa ajili ya wachezaji, kulipa bili za maji, umeme na posho ya kocha Papic kushindwa kutoa.
"Kitendo hicho ni cha aibu kwa klabu kubwa kama Yanga, viongozi wamekaa tu hata hatafuti njia mbadala, baada ya kuondoka Yusuf Manji ambaye alikuwa akisaidia kuongeza fedha kwa ajili ya kulipa mishahara wachezaji, klabu imekuwa na matatizo makubwa zaidi," alisema.
Alisema viongozi hao wameonekana dhahiri kushindwa kuiongoza klabu hiyo, kwa sababu kama inafikia hadi kocha analalamika njaa, hiyo ni hali ya hatari inayoinyemelea Yanga.
Bakari alisema wanampongeza, Papic kwa kuweka wazi kuhusu kinachofanyika ndani ya Yanga, na pia wanamshangaa Katibu Mkuu wao Selestine Mwesigwa kuingilia maisha binafsi ya Papic.
Mwenyekiti huyo, amewataka wanachama wote nchini kuungana kuitisha mkutano ili kuinusuru klabu hiyo na ukata huo kwa kuwa timu yao, inakabiliwa mashindano muhimu ya ndani na nje ya nchi.
Pia aliwataka Wanayanga kuisadia klabu hiyo kwa kutoa michango mbalimbali, itakayoweza kuisaidia timu hiyo katika kipindi hiki kigumu na kuacha malumbano.
No comments:
Post a Comment