21 December 2011

Wamasai waliokiuka mila watembezwa 'utupu'

Na Queen Lema, Arusha 

KATIKA hali isiyo ya kawaida, vijana wa Kimasai 'Morani', juzi waliwatembeza utupu watu watano wa kabila hilo kutoka eneo la Matevesi, mkoani Arusha kwa madai ya
kukiuka mila na desturi za kabila hilo baada ya watoto wao kufanyiwa tohara hospitali.

Morani hao walisema kuwa, kabila hilo halina utamaduni wa watoto wao kufanyiwa tohara hospitali ambapo njia wanayotumia ni ile ya kimila.

Inadaiwa kuwa, Morani hao zaidi ya 2,000 walivamia nyumba za wazazi hao saa 11 alfajiri, kuwatoa nje na kuwatembeza utupu katika maeneo mbalimbali kama adhabu ya kile walichokifanya kwa watoto wao.

Wakizungumza na Majira, baadhi ya wachungaji katika eneo hilo walisema tabia hiyo inapaswa kulaaniwa na wahusika kuchukuliwa hatua kali na Serikali.

“Bila vijana hawa kuchukuliwa hatua, tatizo hili linaweza kuleta madhara makubwa katika maeneo mbalimbali ya mji huu kwa siku za usoni.

“Leo hii viongozi wa Serikali na wanaharakati wanasema taifa lipige vita ugonjwa wa UKIMWI lakini katika tohara ya Kimasai, upo uwezekano mkubwa wa kuongeza maambukizo kwani vifaa vinatumika kwa watu wote.

“Hakuna sheria au kanuni za afya ambazo zinafuatwa, Serikali inapaswa kutoa tamko kukomesha mila hizi ili kupunguza maambukizo,” alisema.

Walisema Morani hao wamekuwa wakisababisha madhara mbalimbali kwa jamii hiyo hasa wanapobaini mzazi kakiuka mila na desturi za tohara kwani wanachukua mali na vitu mbalimbali bila ruhusa ya familia na kusababisha usumbufu.

Awali Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Akili Mpwapwa, alisema hivi sasa wanafanya utaratibu kuhakikisha wanakomesha mila hiyo pamoja na uonevu kwa baadhi ya watu ambao wanapeleka watoto wao katika tohara ya kisasa ili kuwanusuru na maradhi mbalimbali.

Aliongeza kuwa, wote waliohusika katika tukio hilo watachukuliwa hatua kwa kuwa ni kosa la jinai.



3 comments:

  1. Wafungwe iwe fundisho kwa mila za kijinga kama hizi.

    ReplyDelete
  2. Mila ni kitu moja muhimu katika jamii. And the person who said wafungwe need some brain cells.

    The government needs to invest time and money educating traditional culture. This include educating about HIV and transmited diseases.

    ReplyDelete
  3. Masai tribe should learn to change with time and should not be allowed to enjoy stone age life. The tradition they follow is harmful and destructive.

    ReplyDelete