21 December 2011

Ngassa avunja mwiko Yanga

*Aipiga bao, mashabiki vichwa chini

Na Zahoro Mlanzi

HATIMAYE mshambuliaji machachari wa timu ya Azam FC, Mrisho Ngassa amevunja mwiko baada ya kufunga bao moja kati ya mawili dhidi ya timu yake ya
zamani, Yanga katika mchezo maalum wa kuchangisha fedha za kutolea vifaa vya walemavu vilivyokwama bandarini, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, bao lingine lilifungwa na Gaudance Mwaikimba na kuifanya Azam itoke kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 lakini timu hizo zilipata pigo baada ya wachezaji wao, Ngassa na Athuman Idd 'Chuji' kuumia kwa nyakati tofauti.

Ngassa ambaye alijiunga na Azam msimu wa 2009/2010 kwa uhamisho uliodaiwa kuweka rekodi nchini wa zaidi ya sh. milioni 50, tangu ajiunge na timu hiyo hakuwahi kuifunga Yanga mpaka alipofunga katika mchezo huo.

Mshambuliaji huyo alionekana ni mtu mwenye furaha baada ya kufunga bao hilo ambapo alishangilia kwa nguvu zote pamoja na wachezaji wenzake huku akicheza mtindo wa kiduku na kuwafanya mashabi wa Yanga kutoka uwanjani vichwa chini.

Katika mechi hiyo ya jana, Yanga ilianza kwa kujiamini kwa kupiga pasi nyingi zilizowafanya mashabiki wao waliojitokeza kuishangilia, kushangilia muda wote wa kipindi cha kwanza.

Yanga katika kipindi hicho ilionekana kutawala zaidi eneo la kiungo lililokuwa chi ya Chuji na Seif Mohamed 'Kijiko' ambao mara nyingi walionekana kuucheza mpira kwa kupiga pasi nyingi kila upande.

Katika kipindi hicho, Yanga itajutia nafasi ilizopata kupitia kwa Omega Seme, Chuji na Pius Kisambale ambao kwa nyakati tofauti walikosa mabao ya wazi kwa mashuti yao kupaa juu na mengine kutoka nje ya goli.

Azam yenyewe katika kipindi hicho, haikuwa na kazi kubwa zaidi ya kuibana Yanga ambapo dakika ya 43, ilifanya shambulizi la kushtukiza kupitia kwa Ngassa ambaye aliichambua ngome ya Yanga lakini alikwatuliwa na Bakari Mbegu ndani ya eneo la hatari na kuwa penalti.

Penalti hiyo ilikwamisha wavuni na Mwaikimba na kuifanya Azam imalize dakika 45 za kwanza ikiwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili kilianza huku Azam ikifanya mabadiliko kwa kuwatoa Abdulhalim Humud, Kipre Bolou na Kipre Tchetche na nafasi zao kuchukuliwa na Jabir Aziz, Salum Abubakari na Zahoro Pazi ambapo mabadiliko hayo ndio yaliyawamaliza Yanga.

Kuingia kwa wachezaji hao kuliifanya Azam itakate eneo la kiungo ambapo dakika ya 56, Ngassa akaifungia Azam bao la pili akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Abdi Kassim 'Babi' na kumuacha kipa Yaw Berko akiruka bila mafanikio.

Baada ya kufunga bao hilo, hazikupita dakika 10, Ngassa alitolewa nje baada ya kuchezewa vibaya na Nadir Haroub 'Canavaro' na kabla ya tukio hilo, Chuji naye alifanyiwa faulo na Aziz ambaye pia alitolewa nje.

Yanga:Berko, Salum Telela, Stephano Mwasika/Abuu Ubwa, Bakari Mbegu, Canavaro/Chacha Marwa, Kijiko, Chuji/Idrisa Rajabu,Omega Seme/Jeryson Tegete, Pius Kisambale/Hamis Kiiza na Nurdin Bakari.

Azam:Mwadin Ally, Erasto Nyoni, Wazir Salum, Aggrey Morris, Soud Morad, Humud/Aziz,Tchetche/Zahoro Pazi, Kipre Bolou/Salum Abubakari, Mwaikimba, Babi na Ngassa/Khamis Mcha.


No comments:

Post a Comment