19 December 2011

Manji afungua tawi jipya la Yanga G/Mboto

Na Peter Mwenda

ALIYEKUWA Mfadhili wa Yanga, Yusuph Manji, amefungua tawi jipya la Shumato, Mzambarauni, Gongo la Mboto, Dar es Salaam na kuchangia sh. milioni 5 na kusisitiza yeye ni
mfadhili ila ni mwanachama kama walivyo wengine.

Akisoma risala ya tawi hilo ambalo lina wanachama 86 jijini jana, Manji alisema yupo tayari kuendelea kuongeza fedha katika matawi yote nchini yenye nia ya kusajili wachezaji wazuri kama mchezaji wao wa zamani Mrisho Ngassa ambaye kwa sasa anaichezea Azam FC.

Alisema wanachama wa timu hiyo wanafika milioni tisa ambapo kama wote kila mmoja akiamua kutoa sh. 1,000 kwa mwaka, fedha hizo zitatosha kulipa mishahara ya wachezaji na kusajili wengine kutoka mataifa mengine.

Aliwataka wanachama wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuchangia fedha hizo kwani wao ndio wenye uchungu na timu na pia wasome katiba na kuielewa kujua inasema nini katika kuiletea timu hiyo maendeleo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Eugine Mwaiposa ambaye alihudhuria ufunguzi huo, alichangia sh. 100,000 na kuahidi kufungua akaunti ya tawi hilo itakayopewa jina la tawi hilo ili michango na misaada mbalimbali itakayotolewa iweze kuingizwa humo.

Pia Mwenyekiti wa tawi hilo, Aklei Msoma, alisema mikakati ya tawi hilo ni kujenga jengo lao wenyewe na kupata huduma ya kompyutaza kutunza nyaraka zao kwa manufaa ya klabu yao.

1 comment:

  1. YANGA SIKU ZINAYOYOMA MTARUDI MCHANGANI TU KAMA MPAKA SASA HIVI HAMJAFANYA CHOCHOTE. KUMBUKENI ENZI YA SHIRAZ PESA ZILIPOKUWA ZINAMIMINIKA KUTOKA ZANZIBAR. SASA HIVI KUNA MANJI HELA EPA MWISHO WAKE 2015 TUTABANANA HAPAHAPA SIMBA WAMEZOEA HAWANA MJOMBA INGEKUWA SIMBA NDIO WANAPATA HIZO PESA EPA WALLAH MPIRA NCHI HII INGEKUWA NOMA

    ReplyDelete